MBETO: WASIOKIRI UFANISI WA SERIKALI YA RAIS SAMIA NI HAMNAZO

 


Na Mwandishi Wetu, 

Zanzibar.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kuwa watu wanaodai hakuna maendeleo yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, aidha wana matatizo ya uoni au ni "hamnazo".

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya CCM Kisiwandui, Zanzibar.

Mbeto amesema maendeleo makubwa yaliyofanikishwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Dkt. Samia yameishangaza dunia, huku akisisitiza kuwa viongozi makini wanaojua historia ya Tanzania watakiri kuwa kazi kubwa imefanyika kwa ustadi na viwango vya juu.

"Tokea Dkt. Samia achukue kijiti cha uongozi kufuatia kifo cha Dkt. John Magufuli, Serikali yake imeitendea haki nchi hii na watu wake," alisema Mbeto.

Ameeleza kuwa licha ya kuwa miradi mingi ya kimkakati ilianzishwa wakati wa utawala wa Dkt. Magufuli, Serikali ya Awamu ya Sita imeikamilisha kwa mafanikio na hata kuanzisha mingine mipya iliyokamilika pia.

Mbeto alibeza vikali wanaodai hakuna kazi iliyofanyika:

"Watu wakubwa wenye akili timamu wakisema hakuna kilichofanyika, lazima uwaangalie mara mbili. Aidha wana matatizo ya macho au si timamu kichwani – ni hamnazo."

Aidha, amesema Watanzania waliokaa nje ya nchi kwa zaidi ya miaka 30 wanapofika mikoani hukiri wazi kuwa nchi imepiga hatua kubwa kwa muda mfupi."Chama chetu ndicho kilichoasisi Mapinduzi na Uhuru. Kinafahamu hali ya nchi kabla na baada ya ukoloni. Hivyo, kina uwezo wa kupima maendeleo ya kweli," alieleza Mbeto.

Akiwataja baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani vilivyoanzishwa baada ya mwaka 1992, Mbeto alisema ni vigumu kwao kutambua hatua za maendeleo kwa kuwa hawakushuhudia hali ya nchi kabla ya uhuru na mapinduzi.

"Tanzania ya leo si ile ya wakati wa Mjerumani, Mwingereza au Sultan. Sasa ni nchi ya furaha, yenye amani na mafanikio ya kiuchumi," alisisitiza.

Akizungumzia huduma za kijamii, Mbeto alisema hivi sasa kuna vituo vya afya katika kila kata, hospitali za wilaya na mikoa zimeboreshwa kwa dawa na vifaa tiba, huku sekta za kilimo, utalii, uvuvi, barabara na biashara zikipaa.

"Hatupo tena kwenye Tanzania ya kusafiri siku nne kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza au Kigoma. Mtumishi kuhama kwenda Mtwara, Ruvuma au Lindi ilikuwa ni kuacha kazi, lakini leo wanaomba kupelekwa huko," alisema kwa kujiamini.



#raisamiahassan

#maendeleoyatanzania

#awamuyasita

#ccmzanzibar

#mbetokhamis

#tanzaniayakisasa

#ufanisiwakis

erikali

#mapinduziyamiradi

#watanzaniawajivunie


Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.