DAR ES SALAAM.
Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imeibuka mshindi katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam SabaSaba baada ya kushinda tuzo ya muonyeshaji bora katika kipengele cha Mamlaka za Serikali.
Utolewaji wa tuzo hiyo umeshuhudiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa kufunga rasmi maonesho hayo, ikiwa ni kutambua mchango wa PPRA katika kuelimisha wananchi na kuonyesha huduma na mifumo bora ya ununuzi wa umma.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo kwa niaba ya Mamlaka, Meneja wa PPRA Kanda ya Pwani Vicky Mollel amesema ushindi huo unaonyesha jitihada kubwa zinazofanywa na mamlaka hiyo katika kuhakikisha uwazi, ufanisi na uwajibikaji kwenye mchakato wa ununuzi wa umma.
Ameongeza kuwa maonesho ya mwaka huu yamekuwa ya kipekee kwanj yamekuwa na mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi waliotembelea banda la PPRA kutafuta elimu, kujua haki zao na namna wanavyoweza kufuatilia matumizi ya fedha za umma katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Maonesho ya SabaSaba yamehusisha taasisi za serikali, mashirika ya kimataifa na sekta binafsi, na yamelenga kuonyesha bidhaa, huduma na teknolojia mpya sambamba na kutoa elimu kwa jamii juu ya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Hakuna maoni: