Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema Marekebisho ya viwango vya tozo kutoka Shilingi 10,000 hadi Shilingi 2,000 kwa mwaka 2021/2022 ni kiashiria cha Serikali kusikiliza maoni ya wananchi kuelekea kufuta tozo hizo kwa miamala inayofanywa kwa njia ya kieletroniki.
Katika taarifa ya LHRC iliyotolewa leo kwa umma kuhusi tozo za miamala ya simu imesema Baada ya hotuba wa Waziri wa Fedha bungeni kuhusu Makadirio ya Bajeti ya Serikali, 2023/2024 LHRC imebaini uwepo wa mkanganyiko wa wazi juu ya tafsiri ya kufutwa kwa tozo, kinachosemwa na baadhi ya viongozi wa Serikali hakina uhalisia kwenye mizania ya hotuba ya bajeti (rejea ukurasa wa 110 na 111 wa hotuba ya bajeti toleo la kiingereza).
"Mathalani, kauli zinazotelewa na viongozi hao kuwa tozo zimefutwa kwa asilimia mia moja(100%) bila kuelimisha umma kuwa kuna ongezeko la asilimia 50% kwenye tozo ya kutolea fedha hizo (withdrawal levy) kitu ambacho hakisemwi kwa umma kimepelekea watumiaji wa huduma ya kifedha kwa njia ya kielektroniki kuwa na matumaini na matarajio ya kutokuwepo kabisa kwa tozo hizo".
"Ukweli ni kwamba, kwa mujibu wa mawasilisho wa Sheria ya Fedha, 2023 kimependekeza kufutwa kwa tozo za kutuma fedha kwa njia ya kieletroniki huku ikilenga kuacha tozo hizo wakati wa kutoa fedha hizo. Hivyo, mabadiliko haya ya Sheria yanaweza kuwa na athari ya moja kwa moja ya marekebisho ya Kanuni za Tozo za Miamala ya Fedha kwa njia ya Kieletroniki kama ilivyopendekezwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania".
Pamoja, na kufuta tozo za kutuma fedha kutoka kwa mtu moja kwenda kwa mwingine, mabadiliko haya yamehamisha mzigo wa tozo kutoka kwa mtumaji kwenda kwa mtoaji wa fedha hizo. Hivyo, mapendekezo hayo yataongeza gharama kubwa kwa mtoaji wa fedha hizo. Mathalani,mwananchi anayelenga kutuma fedha kwa ndugu, rafiki au jamaa kwa ajili ya kumsaidia jambo fulani atalazimika kutuma na fedha ya ziada ili kumuweza mpokeaji huyo kutoa kiwango kilichokusudiwa au kuacha mpokeaji huyo atoe fedha pungufu tofauti na matarajio ya mahitaji yake.
Aidha LHRC inasisitiza kuwa ni vema Elimu itolewe kwa umma juu ya kiwango halisi cha tozo kilichofutwa na kinachopendekezwa, tofauti na mtazamo uliyopo sasa katika jamii,pia ili kupunguza mzigo kwa mtoaji wa fedha, wanapendekeza mgawanyo wa kupunguzwa kwa asilimia 25% kwa kila upande badala ya ongezeko la asilimia 50% wakati wa kutoa.
"Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Serikali iendane na toleo la hotuba hiyo kwa kiingereza, mathalani ongezeko la tozo ya kutoa pesa kwa asilimia 50% haionekani kwenye hotuba ya Kiswahili, jambo ambalo linawafanya wasomaji kutoelewa taarifa muhimu kuhusu maisha yao".
Hata hivyo, LHRC inasisitiza kuongeza uwazi katika makusanyo na matumizi ya fedha hizo, pamoja na kuongeza uwajibikaji wa wazi kwa wakusanyaji na watumiaji wa fedha hizo ikiwemo kufanyia kazi mapendekezo ya Mdhibiti na Mkuguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
"Serikali ichapishe Tozo za Miamala ya Fedha kwa Njia ya Kieletroniki zenye viwango vipya kutoa tamko rasmi kuhusu tozo hizo". Imesema taarifa hiyo iliyotolewa na Dkt. Anna Henga(WakiIi) Mkurugenzi Mtendaji

Hakuna maoni: