DKT KIKWETE AFURAHISHWA NA NIT KUANZA KUFUNDISHA URUBANI,SERIKALI KUWAPA ENEO KWAAJILI YA KUFUNDISHA MASWALA YA ANGA.
DAR ES SALAAM.
RAIS Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amekipongeza Chuo Cha Taifa ca Usafirisaji (NIT) katika mpango wao wa kuanza kufundisha marubani wa ndege, akisema hatua hiyo itasaidia sana kuongeza watenda kazi katika sekta hii ya anga yenye uhaba mkubwa wa rasilimali watu.
Akiongea katika maaafali ya 39 ya NIT,Dkt Jakaya amesema kuwa ni gharama kubwa kusomesha marubani nje ya nchi.
"Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imenunua ndege mbili kwa ajili ya mafunzo ya urubani, Injini mbili kwaajili ya mafunzo ya uhandisi wa ndege na Cabin Crew mock ups kwa ajili ya mafunzo ya wahudumu wa ndani ya ndege," alisema Rais Mstaafu.
Aliongezea: "Aidha, Serikali imetoa ardhi katika eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) lenye ukubwa wa hekta 60, ambalo litatumika katika kutoa Mafunzo ya Taaluma za Usafiri wa Anga. Nimefurahi sana kuona uwekezaji huu mkubwa na muhimu kwa Chuo chetu, hivyo, nitoe wito kwa Chuo, vifaa hivi ambavyo Serikali imenunua kwa gharama kubwa vitunzwe ili Watanzania wengi wanufaike katika kupata mafunzo."
"Napenda kuwapongeza sana nyote kwa jitihada mlizofanya wakati wote wa masomo yenu hadi kufikia hatua hii ya kutunukiwa vyeti leo hii. Hongereni sana. Ninatambua kuwa tuzo mtakayopata leo ni ya msingi kwenu katika safari ndefu ya kuwa wataalam wazuri na mahiri. Ushauri wangu kwenu msiridhike na ngazi ya taaluma mliyofikia, endeleeni kutafuta maarifa zaidi ili Taifa liwe na wataalam wa kutosha na wenye sifa zote zinazohitajika katika sekta ya Uchukuzi na Usafirishaji. "
Kwa Wanafunzi Mnaoendelea na Masomo, alisema:"Katika zama hizi ambapo kuna mabadiliko makubwa ya teknolojia hasa dunia inapoingia kwenye Mapinduzi ya Nne ya Viwanda (4th Industrial Revolution), ubunifu ni jambo muhimu kwa Nchi yetu katika kujenga uchumi imara na stamihilivu. Hivyo, Wanafunzi mnaoendelea na masomo kuweni wabunifu na kusoma kwa bidii ili mtakapohitimu masomo yenu muweze kuwa na maarifa na ujuzi wa kutosha. "
Alisema kuwa amefarijika sana kusikia kwamba Chuo kimeendelea kutanua wigo wa kutoa mafunzo katika sekta hii muhimu ya Uchukuzi, ikiwa ni pamoja na kujiimarisha katika Njia zote za Usafirishaji yaani Usafiri wa Anga, Majini, Reli, Barabara na usafiri kwa njia ya mabomba.
"Nimefarijika kusikia kuwa Chuo kikombioni kuanza kutoa Mafunzo ya Urubani. Mafunzo haya ni muhimu sana kwa Taifa letu kwani yatapunguza mzigo kwa Serikali na Wazazi wa kugharamia mafunzo haya nje ya nchi ambayo hutolewa kwa gharama kubwa, " alisema Dkt Kikwete
Vilevile, Jakaya alipata wasaa wa kuzindua Kitabu ambacho kimeeleza historia ya Chuo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1975 hadi kilipofika hapa.
"Nimefurahi kuona sasa historia ya Chuo chetu imetunzwa vema kwani inatusaidia kujua tulikotoka, tulipo sasa na wapi tuanataka kufika. Aidha, kitabu hiki kinatunza historia ya Chuo kwa faida yetu, vizavi vijavyo na kwa kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu, " alisema.
Naye, Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile alisema kuwa Katika kutekeleza wajibu wetu wa kusimamia Chuo, Wizara imefanikiwa kusimamia uboreshaji wa miundombinu na mazingira ya kufundishia na kujifunzia; uboreshaji wa mafunzo yanayotolewa na Chuo; pamoja na kuimarisha rasilimali watu ya Chuo
Usimamizi huu unalenga kukiwezesha Chuo kufikia malengo ya uanzishwaji wake, ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa kama yalivyoainishwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025.
"Chuo chetu kinatambua mapinduzi anuai ambayo Serikali ya Awamu ya Sita (6) imeendelea kuyafanya kwa kuanzisha miradi mbalimbali katika sekta ya Uchukuzi ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mipango mbalimbali ya nchi ikiwemo Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo, Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025, Sera ya Taifa ya Uchukuzi ya mwaka 2003, pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020," alisema.
Alisisitiza kuwa baadhi ya miradi hiyo ni ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), Ununuzi wa Mabehewa na Injini za treni za kisasa, ujenzi wa Meli, upanuzi wa Bandari, ujenzi na upanuzi wa Viwanja vya Ndege, ununuzi wa Ndege,, ujenzi na upanuzi wa barabara pamoja na ujenzi wa Bomba la Mafuta Gafi kutoka Hoima, Uganda kwenda Tanga, Tanzania.
"Mapinduzi haya yameongeza mahitaji ya Rasilimali Watu yenye weledi wa hali ya juu katika Sekta ya Uchukuzi nchini na ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika," alisema.
Naibu Waziri alitabanaisa "Hii inakifanya Chuo kubuni na kutoa mafunzo yanayoendana na mahitaji ya soko ili kutoa wahitimu bora katika nyanja zote za Usafirishaji (Barabara, Reli, Anga, Maji na Bomba). Hivyo basi, katika Mpango Mkakati wa Nne wa Chuo wa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026), Chuo kitaendelea kuimarisha utoaji wa mafunzo yanayolenga kuzalisha wataalam wenye ujuzi katika sekta ndogo zote tano za usafirishaji kwa ajili ya ukuaji endelevu wa miradi hii ambayo itachochea kwa kasi ukuaji wa Uchumi wa nchi yetu."
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo Dr Zainabu Mshana amesema kuwa Chuo kimeendelea kuwajengea uwezo wahadhiri na watumishi wake kwa kuwapeleka masomoni ili kuimarisha kiwango cha maarifa na ujuzi wao ambapo katika mwaka wa masomo 2023/2024 jumla ya watumishi 71 wapo masomoni.
Amesema kuwa kati ya hao, watumishi 39 wanasoma ngazi ya shahada ya uzamivu (PhD), 24 wanasoma shahada ya uzamili, mtumishi mmoja (1) anasoma shahada ya kwanza, Watumishi watatu (3) wanasoma Mafunzo ya Urubani na Watumishi wanne (4) wanasoma Mafunzo ya Leseni ya Matengenezo ya Ndege.
Vilevile, aliongezea kuwa katika kuimarisha na kurahisisha utendaji kazi, Chuo kimefanikiwa kuhuisha muundo wake wa utumishi, ambao uliidhinishwa na Mheshimiwa Rais tarehe 17 Novemba 2022 na umeanza kutekelezwa Mwezi Oktoba 2023.
"Kwa upande wa taaluma, Muundo huu una Vitivo vitano (5), Kurugenzi mbili (2), Idara 14, Vitengo sita (6) na Vituo vinne (4). Kwa upande wa Utawala, Muundo una Kurugenzi (5) na Vitengo vinne (4), "alisema.
Aliongezea kuwa Chuo kimefanikiwa kufanya maboresho ya Muundo wake wa Utumishi kwa kuongeza kada za wakufunzi wa usafiri wa anga na wahandisi wa matengenezo ya ndege ili kuendena na matakwa ya sekta ya usafiri wa anga. Muundo huu umeanza kutekelezwa mwezi Oktoba 2023.
Pamoja na hayo, Chuo kimefanikiwa kuidhinishiwa Muundo wa motisha ili kuboresha maslahi ya watumishi na kuongeza ufanisi wa kazi katika shughuli mbalimbali za Chuo. Muundo huu umeanza kutekelezwa mwezi Julai 2023.
"Chuo kina mikakati endelevu ya kutayarisha Rasilimali Watu watakaokidhi mahitaji ya soko la ajira kwenye sekta ya Uchukuzi na Usafirishaji hasa kwa kuzingatia utekelezaji wa mageuzi makubwa ya kiuchumi ambayo Serikali ya Awamu ya sita (6) inayafanya, " alisema.
Alitaja Mikakati hiyo ni Kuanzisha na kuhuisha mitaala ya kozi za mafunzo mbalimbali kuanzia ngazi ya stashahada hadi shahada ya uzamili kuendana na mahitaji ya soko la ndani na la nje ya nchi
Na vilevile kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia ikiwa ni pamoja na ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya madarasa, karakana, maabara, ofisi na ununuzi wa vifaa vya mafunzo vinavyoendana na mabadiliko ya teknolojia duniani.




Hakuna maoni: