SERIKALI YAFUTA TAASISI NA MASHIRIKA UMMA 04 NA KUYAUNGANISHA 16,HUKU IKISISITIZA KUWA MCHAKATO HUO MWENDELEZO.
Na Emmanuel Kawau,
Dar es salaam.
Waziri wa Wizara ya Mipango na Uwekezaji Prof Kitila Mkumbo amesema Serikali imeridhia na kuelekeza kuunganishwa kwa mashirika na taasisi 16 na kufuta mashirika na taasisi za umma nne.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es salaam Prof Mkumbo amesema Serikali imefikia uamizi huo ili kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika shughuli za uwekezaji na biashara.
"Katika kutekeleza hili, sekta ya umma itajielekeza katika maeneo yasiyovutia uwekezaji wa sekta binafsi. Mashirika ya umma yatahimizwa kuwekeza katika maeneo ya kimkakati kulingana na majukumu yao. Aidha, Serikali itaelekeza rasilimali nyingi kwenye miradi mikubwa yenye matokeo ya muda mrefu, hususani, ile isiyovutia sekta binafsi kuwekeza".
Pia Serikali imefikia uamuzi huo ili kupunguza mzigo wa kuendesha mashirika ya umma yanayohitaji ruzuku ya serikali katika kujiendesha,mashirika na taasisi zenye mwingiliano na mfanano wa malengo na majukumu yataunganishwa na kuunda shirika au taasisi moja.
Prof Mkumbo ameyataja Mashirika na Taasisi za umma zinazounganishwa ambayo ni Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (National Identification Authority-NIDA) na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Registration, Insolvency and Trusteeship Agency -RITA) yanaunganishwa na kuunda taasisi moja inatayohusika na utambuzi wa matukio muhimu maishani. Lengo ni kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais, ya kuwa na namba moja ya utambulisho (Single Identification Number).
Benki ya Kilimo Tanzania (Tanzania Agricultural Development Bank -TADB) na Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (Agricultural Inputs Trust Fund -AGITF) zinaunganishwa ili kuwa na taasisi moja itakayohusika na mikopo na
ugharamiaji wa maendeleo ya kilimo nchini.Bodi ya Chai inaunganishwa na Wakala wa Maendeleo ya Wakulima Wadogo wa Chai Tanzania (Tanzania Smallholders Tea Development Agency -TSHDA) zinaunganishwa ili kuwa na bodi moja. (Bodi ya chai).
Pia Bodi ya Nyama inaunganishwa na Bodi ya Maziwa zinaunganishwa ili kuunda taasisi moja ya kuendeleza na kusimamia mazao ya mifugo yakiwemo ya nyama na maziwa Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CARMARTEC), Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO) na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) zinaunganishwa ili kuunda taasisi moja.Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kinaunganishwa na Mamlaka ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) ili kuunda taasisi moja itakayoratibu uwekezaji wa sekta binafsi wa ndani na kutoka nje ya nchi.
Taasisi ya Utafiti wa Chai Tanzania (Tea Research Institute of Tanzania -TRIT),Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku Tanzania (Tobacco Research Instititute of Tanzania -TORITA) na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (Coffee Research Institute of Tanzania – (TACRI) zinaunganishwa na kuwa sehemu ya muundo wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).
Kwa upande wa Mashirika na Taasisi za Umma zinazofutwa/kuvunjwa ni Shirika la Uzalishaji la Jeshi la Polisi (Tanzania Police Force Corporation Sole -TPFCS) linafutwa.Taasisi ya Chakula na Lishe (Tanzania Food and Nutrition Centre – TFNC) inafutwa.Shirika la Elimu Kibaha (Kibaha Education Center - KEC) linavunjwa na kuunda Shule ya Sekondari Kibaha ama kwa jina ambalo Mamlaka husika zitaamua na Chuo Cha Ufundi.
"Kwa uamuzi huu hospitali ya Tumbi Kibaha haitakuwa tena sehemu ya Shirika la Elimu Kibaha bali hospitali ya Mkoa wa Pwani.Msajili wa Hazina ameshaelekezwa kukamilisha taratibu husika za makabidhiano na Wizara ya Afya"
Bodi ya Pareto inafutwa na shughuli zake zitahamishiwa katika Mamlaka ya Usimamizi wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CEREAL AND OTHER PRODUCE REGULATORY AUTHORITY-COPRA)
"Katika mchakato huu, mambo matatu yafuatayo yatazingatiwa:Hakuna mtumishi atakayepoteza ajira yake Maslahi yote watumishi ya umma katika mashirika na taasisi husika yatalindwa na kuzingatiwa kikamilifu kwa kuzingatia sheria na kanuni za utumishi wa umma. Izingatiwe kuwa katika mashirika na taasisi nyingi za umma na serikali kwa ujumla kuna upungufu mkubwa wa watumishi wa umma Kwa hivyo watumishi wote
ambao mashirika na taasisi zao zinaguswa na zoezi hili watapangiwa kazi zingine katika utumishi wa umma na maslahi yao yatazingatiwa ipasavyo" Amesema Prof Mkumbo na kuongeza kuwa
"Mchakato wa kufuta na/au kuunganisha mashirika na taasisi za umma utazingatia sheria ambazo zimeanzisha taasisi hizo. Ni kwa sababu hii,uamuzi ninaoutangaza hapa tayari ulishawasilishwa kwa Mawaziri husika ambao ndio wenye nyezo husika (Ministerial Instrument Holder) kwa hatua zao stahiki".
Prof Mkumbo amesisitiza kuwa Mawaziri husika wameshaelekezwa kuhakikisha kuwa mchakato wa kufuta na/au kuunganisha mashirika na taasisi za umma zilizotangazwa uwe umekamilika ndani ya mwaka huu wa fedha.Mageuzi katika utendaji na uendeshaji wa Mashirika ya Umma ni zoezi endelevu.Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya kupima na kutathimini utendaji wa mashirika na taasisi za umma kwa lengo la kuongeza tija katika maendeleo ya nchi.
"Serikali kuendelea kugharamia mashirika ya umma ambayo majukumu yao ya msingi ni kutoa huduma kwa umma na ambayo majukumu hayo kwa asili yake lazima yatolewe na sekta ya umma".

Hakuna maoni: