JESHI LA POLISI,KIKOSI CHA USALAMA BARABARANI KIMETANGAZA KUANZA OPERASHENI YA KUKAMATA MAGARI NA PIKIPIKI ZINAZOFUNGWA VING'ORA NA VIMULIMULI KINYUME NA SHERIA.
Na Emmanuel Kawau,
Dar es salaam.
Jeshi la Polisi kikosi cha usalama Barabarani kimetangaza rasmi kuanza oparesheni kabambe ya kukamata magari na pikipiki zote ambazo si za dharura na zimefungwa ving'ora bila kuzingatia utaratibu wa sheria ya usalama barabarani.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Kamanda wa kikosi cha Usalama Barabarani, DCP Ramadhan Ng'anzi amesema kuwa Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani kimepiga marufuku wamiliki na madereva wote nchini kuweka Ving'ora, Vimulimuli, Namba bandia na taa za kuongezwa kwenye magari na pikipiki kama kuna ulazima wa kufanya hivyo basi wanatakiwa kuomba ridhaa ya kupata kibali cha kufanya hivyo kwa Waziri wa Mambo ya Ndani.
Ameongeza kuwa ni kosa kwa mtu yoyote kufunga king'ora katika gari au pikipiki bila kuzingatia utaratibu wa kisheria na kanuni za usalama barabarani zilizowekwa kwa mujibu wa sheria na hatua kali zitachukulia dhidi yao ikiwemo kupelekwa mahakamani.
"Wapo baadhi ya wananchi ambao wamegeuza ving'ora kuwa fasheni katika magari au pikipiki zao, tukumbuke kuweka king'ora cha aina yoyote katika gari au pikipiki ni lazima ufuate sheria tutawakamata kuanzia leo wote watakaokaidi agizo hili na tutawachukulia hatua"amesema Kamanda Ng'anzi.
Aidha, amesema kuwa,kuna baadhi ya watu, makampuni na taasisi mbalimbali zimekuwa zikivunja sheria ya usalama barabarani, na wanastahi adhabu ikiwemo ya kulipa faini ya tozo za makosa ya usalama barabarani au kuwekwa mahabusu na kuandaliwa mashtaka na kupelekwa mahakamani au vyote kwa pamoja.
Aidha, amesema kuwa ni kosa kisheria kufunga taa zenye mwanga mkali zinazoongezwa kwenye magari au pikipiki yaani spot light na led bar wanafunga kama urembo kwenye magari na pikipiki na wanatakiwa wavitoe mara moja kwani wamefunga kwa kinyume cha sheria, taratibu na kanuni za usalama barabarani.
"Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani litafanya oparesheni kali kudhibiti ufungwaji wa taa zinazoongezwa kwenye magari na pikipiki, kuna watu wanaweka Taa za kuongezwa kwenye magari, nyuma ya magari makubwa hususani malori, wananchi wenye tabia hii waache mara moja kwani ni kinyume cha sheria"
"Iwapo magari hayo yamewekwa taa hizo kutoka kiwandani basi zinaruhusiwa ,hata hivyo matumizi yake yawe ni sehemu za migodi tu na kwenye mapori wakati wa uwindaji na si vinginevvyo,ila anapotoka sehemu hizo aweke kava za kuzuia mwanga mkali barabarani kwani mwanga huu unaweza kusababisha uoni hafifu kwa watumiaji wengine wa barabara" amesema Kamanda Ng'anzi.
Ameongeza pia ni kosa kisheria gari au pikipiki kubandikwa namba bandia zisizo na usajili, ambapo baadhi ya watu wamejenga utamaduni ambao wanajihalalishia kuwa ni sheria kuweka namba bandia kwenye magari, hivyo wanatakiwa watoe mara moja namba hizo kabla ya oparesheni kuanza.
Jeshi la Polisi, Kikosi cha usalama barabarani linatoa wito kwa wamiliki na madereva wote nchini kutoweka vingora,vimulimuli,namba za bandia na taa za kuongezwa kwenye magari na pikipiki kama kuna ulazima wa kufanya hivyo basi wanatakiwa kuomba kibali kutoka kwa Waziri wa mambo ya ndani.

Hakuna maoni: