FCC, TRADEMARK AFRICA WASAINI MKATABA WA MIAKA MITATU WA MASHIRIKIANO.


NA MWANDISHI WETU,

DAR ES SALAAM .

TUME ya Ushindani (FCC) na TradeMark Africa (TMA) wamesaini mkataba wamashirikiano wa miaka mitatu katika kuunga mkono utekelezaji wa shughuli za tume hiyo yaani (Partner Support Agreement -PSA) katika kulinda na kushaghisha ushindani katika kulinda mlaji na kudhibiti biashara bandia.


Tukio hilo la mkataba wa awali umegharimu kiasi cha Tsh. 1.56 Bilioni, limefanyika mapema leo Mei, 27, 2024 Dar es Salaam ambapo limeshuhudiwa na watendaji wa pande zote mbili mbele ya Waandishi wa Habari.

Awali Mtendaji Mkuu wa FCC, Bw. William Erio amebainisha kuwa TMA wamekuwa wakifanya mambo mengi ikiwemo kuhakikisha shughuli za ukuaji wa kibiashara na Tanzania inakuwa na sehemu nzuri ya uwekezaji.

Mtendaji mkuu huyo William Erio amebainisha kuwa, katika mkataba huo, TMA watahakikisha shughuli za utendaji za FCC zote zinakwenda Kidijitali, Kuboresha kwa kiwango kikubwa miundombinu ya Tehama na taasisi, na mwisho kuwa na mafunzo kwa wafanyakazi katika kuhakikisha wanafanya kazi vizuri na kwa haraka zaidi na kwa ufanisi unaotarajiwa na wawekezaji.

“Matokeo yake ni kwamba muda wa kushughulikia maombi mbalimbali ya kibiashara utapungua sana na gharama za utekelezaji pia zitakuwa ndogo.

Na tunaamini pia hii itaendana sambamba na muelekeo wa awamu ya sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye amekuwa anasafiri katika nchi mbalimbali akipigania nchi yetu ipate maendeleo ya kiuchumi kwa kuvutia wawekezaji na wafanyabiara kuja kuwekeza na kufanya biashara ndani ya nchi yetu,

Lakini pia kuiwezesha nchi yetu kunufaika na fursa za kufanya biasara katika masoko mbalimbali ikiwemo AfCFTA, Jumuiaya ya Afrika Mashariki, Jumuiya za kiuchumi Kusini mwa Afrika (SADC), na zingine nyingine.’’ Amesema Bw. William Erio.


Aidha, amesema mkataba huo ni katika kuhakikisha wanaelekea katika Tanzania ambayo Rais anaikusudia ifikiwe, itafikiwa na maendeleo kwa ujumla wake yatapatikana.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa Trademark Africa, Bw Elibariki Shammy ameshukuru Serikali ya Tanzania pamoja na FCC kwani anaamini mkataba huo unaenda kujenga utendaji kazi bora huku akibainisha kuwa, ni muhimu kwa malengo ya kimkakati ya kuchochea ukuaji wa biashara ambao ni endelevu na shirikishi.

Trademark Africa inatekeleza mradi huo ambao umefadhiliwa na Serikali ya Uingereza, Jumuia ya Madola, Ireland na Norway.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.