DAR ES SALAAM.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa habari za mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vingine kwa ujumla ili kuhakikisha kuwa sekta hii inaendelea kukua na kuchangia katika kuleta maendeleo kwa Taifa.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Mei 21, 2024) katika Kongamano la Jumuiya ya Wanahabari wa Mitandaoni ya Kijamii (JUMIKITA) kuhusu mafanikio ya miaka mitatu ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam.
"Serikali haina namna ya kuwatenganisha Jumuiya hii na Mafanikio ya Serikali yetu. Tunatambua, Tunathamini na tunashukuru kwa kazi nzuri mnayoifanya na endeleeni kufanya kazi kwa uhuru wa kutokiuka taratibu za kitaifa na kimataifa-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
“Kupitia vyombo vya habari, hasa vya mitandao ya kijamii, tumeweza kuwahabarisha wananchi kuhusu shughuli na mipango ya Serikali, na kuhamasisha ushiriki na ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli na mipango hiyo.”
Pia mezutaka mamlaka zinazohusika na usimamizi wa sekta ya habari ziendelee kusimamia vyombo vya habari vizingatie maadili na kujiepusha na uchapishaji wa taarifa na picha zinazochochea uvunjaji wa maadili, mila na desturi za Kitanzania.
Ameongeza kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kuboresha Sheria na Miongozo inayosimamia sekta ya habari ili kuweka mazingira wezeshi kwa wanahabari kufanya kazi zao kwa uhuru na kwa kuzingatia maadili, tamaduni na haki za watu wengine.
“Katika kipindi hiki cha miaka mitatu toka Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani amewezesha kukua kwa sekta ya habari na hasa ongezeko la watumiaji na wasomaji wa habari kupitia mitandao ya simu.”
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali imeandaa Mkakati wa Mawasiliano wa Taifa ili kuhakikisha wadau katika ngazi zote wanapata taarifa za kutosha na wanashiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi na kuimarisha mawasiliano ya Serikali.
Hakuna maoni: