SERIKALI YAITAKA TUCTA KUWEKA MIKAKATI YA KUWAFIKIA NA KUWAELIMISHA WAFANYAKAZI KUTOKA SEKTA ISIYO RASMI NCHINI.
DAR ES SALAAM.
Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu kazi vijana, ajira na wenye ulemavu, Deogratius Ndejembi ametoa rai kwa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania TUCTA kuweka mipango madhubuti ya kuwafikia na kuwapa elimu wafanyakazi wanaofanya kazi katika sekta isiyo rasmi waone umuhimu wa kujiunga katika vyama vya wafanyakazi ili wapate mazingira mazuri ya ufanyaji kazi na kupata huduma stahiki.
Ndejembi ametoa agizo hilo leo jijini Dar Es Salaam wakati akifungua mafunzo kwa viongozi wakuu wa vyama vya wafanyakazi vinavyoratibu sekta isiyo rasmi ambapo amesema serikali inatambua na kuthamini sekta isiyo rasmi kwa kuwa ndio nyenzo kuu inayosukuma ukuaji wa uchumi wa nchi.
Aidha Ndejembi amesema Serikali imeweka mazingira mazuri ya kuhakikisha kwamba sekta isiyo rasmi inapata mitaji hatua itakayofanya uwepo wa ongezeko la wajasiriamali wengi na kukuza biashara.
Naye Katibu Mkuu wa TUCTA, Hery Mkunda amesema lengo la mafunzo hayo kwa viongozi hao ni kuwapa uwezo ,maarifa na fursa mbalimbali ambazo wafanyakazi kutoka katika sekta isiyo rasmi wanaweza kuzipata na matarajio makubwa ya mafunzo ni kuona wafanyakazi wanaofanya kazi katika sekta isiyo rasmi wanajiunga na vyama vya wafanyakazi .
Mafunzo haya yamehudhuriwa pia na Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Ndg. Tumaini Nyamhokya ambaye alimkaribisha Mgeni Rasmi na kutumia nafasi hiyo kumshukuru Mhe. Waziri kwa ushirikiano mkubwa ambao amekuwa akiutoa kwa Shirikisho hilo tangu kushika nafasi hiyo na kuahidi kuwa wapo tayari kuendelea kushirikiana katika mambo mbalimbali ili kuendelea kuboresha maslahi ya Wafanyakazi nchini.
Mafunzo haya ni ya siku mbili yameandaliwa na TUCTA na ZATUC kwa kushirikiana na ILO ACTRAV yanalenga kuongezea ufahamu na utambuzi wa mifumo mbalimbali iliyopo ya kinga za jamii (Labour Protection) kwa Viongozi wakuu wa Vyama vya Wafanyakazi wanaoratibu Sekta isiyo rasmi ili kuweza kuzitumia kuboresha maisha ya Wafanyakazi wa kundi hili muhimu.
Hakuna maoni: