DOYO ATANGAZA KUWANIA NAFASI YA MWENYEKITI WA CHAMA ADC.

DAR ES SALAAM.

Aliyekuwa Katibu mkuu wa Chama cha Alliance for Democratic Change Hassan Doyo ameibuka kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Chama hicho ambapo nafasi hiyo imeachwa wazi na Hamad Rashid ambaye muda wake ulimalizika hivi karibuni.

Akitangaza kuwania kiti hicho mbele ya Waandishi wa Habari mapema leo Juni 6, 2024 jijini Dar es Salaam Doyo Amesema achukua rasmi fomu siku ya tarehe 11/06/2024.

"Sababu kubwa ambayo imenifanya kuwania nafasi hiyo ni kutokana na kuwa na uzoefu wa kutosha baada ya kulelewa vema na aliyekuwa Mwenyekiti wetu, Hamad Rashid". Amesema Doyo na kuongeza kuwa.

"Nimekaa na Mwenyekiti wetu kwa muda wa miaka 10 nikiwa Katibu Mkuu na sikuwahi hata siku moja kutofautiana naye na nimejifunza mengi ikiwemo suala uvumilivu na kuheshimu Katiba, ambayo ameitekeleza kwa vitendo kwa kuondoka madarakanj kwa mujibu wa sheria tulizojiwekea," amesema.

Aidha Doyo katika chama hicho ameweza kufanya kazi na viongozi mbalimbali, akiwemo Mwenyekiti wa kwanza, Said Bilal wakati akiwa Mkurugenzi wa Habari.Pia amefanya kazi na Lucas Silimu aliyekuwa Katibu Mkuu wakati huo, Mama Lydia Bendera (Katibu Mkuu), Juma Kilagai (Katibu Mkuu) na Abubakari Rakesh.

Hivyo amewataka wanachama wa chama hicho kutokuwa na wasiwasi naye katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Juni 27 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Ameendelea kwa kubainisha kuwa endapo atafanikiwa kushika nafasi hiyo, moja ya mikakati yake ni kukiimarisha chama kiwe kikuu cha upinzani na kifanye vizuri bungeni na kuisimamia vema Serikali maslahi ya Watanzania.

Pia atabeba agenda tatu ambazo ni mabadiliko ya sheria, mabadiliko ya ajira ambayo itafanya wanafunzi kupata elimu Bora itakayowasaidia maishani na agenda ya maisha Bora kwa Mtanzania.

Pia wakati akitangaza kuwania nafasi hiyo aliambatana na anayegombea umakamu uenyekiti, Scolastica Kahana aliyekuwa mgombea ubunge wa chama hicho katika Jimbo la Kibaha Mjini katika uchaguzi wa mwaka 2020.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.