GAWIO LA TPA LAWAKOSHA WADAU.


Na Mwandishi Wetu, 

Dar es Salaam

WADAU mbalimbali nchini wamezungumzia gawio la Sh bilioni 153.9 kwa serkali kuu kwa mwaka 2023/24 lilitolewa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) ni matokeo ya maboresho makubwa yanayoendea na uongozi makini wa mamlaka hiyo.

Mbali ya maboresho na umakini wa uongozi wa mamlaka, uamuzi usioyumba wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan wa kukaribisha makampuni ya kimataifa yenye uwezo na uzoefu wa kusimamia na kuendesha shughuli za bandari duniani kuja kuwekeza kwenye bandari za Tanzania.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Raphael Maganga amesema uwekezaji wa miundombinu bandarini umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi wa kiutendaji na hatimaye kupaisha mapato yake na hatimaye kutoa gawio kubwa kwa serikali kuu kwa kipindi tajwa.

“Mifumo yake kisasa inasomana vizuri na ile ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) sambamba na ile taasisi zingine. Kwa gawio la Sh bilioni 153.9 si haba ni matokeo chanya ya uwekezaji na mchango mkubwa wa sekta binafsi,” amesema Maganga na kuipongeza mamlaka hiyo.

Kwa mujibu wa bosi huyo wa sekta binafsi hapa hapa nchini, maono ya Rais Dk Samia na uwezo wa menejimenti ya TPA kutafsiri maono hayo kwa vitendo yamechangia kuongeza ufanisi ikiwemo kuongezeka kwa mzigo unaopita bandarini.

“Idadi ya mzigo inayopita katika Bandari ya Dar es Salaam umeongezeka katika kipindi cha miaka hii mitatu kwanini maboresho makubwa yaliyofanywa yameweza kuvutia mziigo uliokuwa unapita Bandari za Mombasa na Durban sasa unapita hapa,” amesema Maganga.

Wakili Msomi na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Kampasi ya Mbeya, Dk Tasco Luambano amesema TPA imeweza kutoa gawio ambalo hakuna taasisi yeyote ambapo imetoa gawio mwaka 2023/24 imeweza kufika hata nusu yake na hivyo kufunga kabisa midomo ya wakosoaji.

“Niliwahi kuzungumzia faida zitakapatikana kutokana na serikali kuwakaribisha washindani tofauti kuja kuendesha shughuli za bandari. Gawio la TPA kwa serikali kuu inadhirisha kuongezeka kwa ufanisi ambao unachangia kuongezeka kwa mapato,” amesema Dk Luambano.

Dk Luambano amesisitiza kuwa Bandari kama lango kuu la uchumi ameshauri wadau kutoka sekta binafsi kushirikiana na serikali kuwekeza kwenye miundombinu ya reli na barabara ilikubiliana na uwingi wa mzigo kwenye bandari.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dk Godwill Wanga mbali ya kuipongeza TPA kwa kuwa kinara kwa kutoa gawio nono kwa serikali amesema hiyo ni ushuhuda kwa kuboreka kwa mazingira ya kufanya biashara na kuvutia uwekezaji hapa nchini.

“Juhudi kubwa zimefanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk Samia kuhakikisha mazingira ya kufanya biashara yanakuwa rafiki na wezeshi kwa makapuni binafsi na mashirika umma kufanya biashara na uwekezaji,” amesema Dk Wanga.

Serikali imepokea gawio la jumla ya shilingi bilioni 637 kutoka taasisi na mashirika 145 ambapo kati ya pesa hizo shilingi 278 zilitolewa na taasisi zinazofanya biashara (Business entities) na shilingi 358 ni kutoka taasisi za udhibiti (Regulatories)

Akipokea gawio hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Dk Samia alisema serikali inataka kupokea gawio la kutosha kutoka kwa taasisi zote kuanzia mwakani na kuelezea matumaini yake kuwa anategemea TPA itatoa zaidi ya mara mbili kutokana na kushimiri kwa biashara.

Katika kufanya kazi kiushindani na kujiimarisha kibiashara, TPA imeingia mikataba ya kiundeshaji kwenye baadhi ya gati zake katika Bandari ya Dar es Salaam ambapo Kampuni ya DP World kutoka Dubai inaendesha gati namba 4 hadi 7 gati namba 0 hadi 3 zinaendeshwa kwa pamoja kati ya Mamlaka ya Bandari na Kampuni ya DP World.

Mbali ya DP World, kampuni ya Adani International Ports Holding Limited ( AIPH) ya India inaendesha gati namba 8 hadi 11 zamani zilizokuwa zinaendeshwa na iliyokuwa kampuni ya kimataifa ya Tanzania International Containers Terminal Services (TICTS) ambayo mkataba wake wake uendeshaji ulimalizika.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.