DAR ES SALAAM.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson Msigwa amesema Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya inaandaa mpango wa kufanya mazoezi nchi nzima ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza kwa Watanzania.
Msigwa amesema hayo leo Juni 23, 2024 Jijini Dar Es Salaam kwenye maadhimisho ya siku ya Yoga kimataifa ambapo amewasisitiza Watanzania wajenge tabia ya kufanya mazoezi ili kuimarisha afya.
“Ndugu zangu Watanzania tunapoungana kusherehekea siku hii naomba kutoa wito kwa kila mmoja wetu kila siku inayoenda kwa Mungu kujiuliza nimefanya mazoezi? Yoga ni moja ya mazoezi rahisi na mepesi unayoweza kufanya mahali popote, ambao wanasema hawawezi kukimbia jifunzeni Yoga itawasaidia” Amesema Msigwa.
Mazoezi ya Yoga yanahusisha namna ya kupumua, kulegeza viungo na misuli ya shingo, mabega, mikono na miguu, namna ya kusimama, namna ya kukaa mkao mdogo wa kuegemea na kufuatiwa na tafakari fupi.
Maadhimishio hayo ya siku ya Yoga kimataifa yamebebwa na kaulimbiu isemayo Yoga kwaajili yako na kwa jamii nzima.
Hakuna maoni: