Na Shamu Lameck,
Ifakara.
Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) limeanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa tuta la kuzuia maji ya mto lumemo uliopo kwenye Halmashauri ya mji wa Ifakara mkoani Morogoro.
Akizungumza Juni 15,2024 Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe.Dastan Kiobya amepongeza jitihada za serikali za kuwaondolea adha ya maji kuingia kwenye makazi kutokana na mto kujaa wakati wa masika na kusababisha maji kwenda kwenye makazi ya watu.
Utekelezaji wa mradi huu utakuwa msaada mkubwa sana kwa kusaidia kuondoa changamoto ya maji kujaa kwenye makazi ya watu.
"Niwaombe wananchi wote kutoa ushirikiano ili kazi hii ya ujenzi wa tuta iweze kutekelezwa na kukamilika kwa wakati ili kuondoa shida ya maji kujaa kwenye makazi yetu wakati wa masika kutokana na mto kujaa", ameeleza Mhe. Kiobya
Vile vile aliwasisitiza viongozi kuendelea kusimamia mradi huu na kuangalia watu waliyokuwa wanafanya shughuli za binadamu kwenye hifadhi ya mto wanaacha mara moja.
"Kazi yetu ni kulinda vyanzo vya maji, hivyo viongozi wote tuhakikishe watu waliopo ndani ya mita 60 wanaondoka" amesema Mhe. Kiobya.
Aidha, aliwaelekeza watendaji wote wa Kata kushirikiana na wataalam wa bonde la mto Rufiji kubainisha na kuweka alama ya mita 60 za hifadhi ya mto, lengo likiwa kuepusha madhara yaliyotokea wakati wa masika yasitokee tena kwenye Wilaya ya Ifakara.
Kwa upande wake Meneja mazingira kutoka TANESCO ndugu Tluway Sappa amesema kuwa, ujenzi wa tuta la Mto Lulemo utaenda kuongeza maji yanayoingia kwenye mto Kilombero.
"Mto Lumemo unachangia asilimia 35 ya maji kwenye mto Kilombero, ambapo mto Kilombero nao unachangia asilimia 65 ya maji kwenye maji yanayoenda kwenye bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere . Hivyo ujenzi wa tuta hili utaenda kuongeza maji kwenye bwawa la Julius Nyerere, na kuongeza uhakika wa maji nyakati zote", amesema Sappa.
Naye msimamizi wa bonde la rufiji Mha. Emmanuel Lawi amewahakikishia wakazi wa Ifakara kuwa kazi ya ujenzi wa tuta itakamilika ndani ya kipindi cha miezi miwili,kabla ya kuanza awamu ya pili ambayo itahusisha upande wa pili wa Mto Lulemo.
Hakuna maoni: