Na Selemani Msuya
WAKATI Juni 12, 2024 dunia ikitarajia kuadhimisha siku ya utumikishwaji wa mtoto duninia, takwimu zinaonesha zaidi ya watoto milioni 5 wanatumikishwa nchini Tanzania, huku watoto milioni 4.8 wakiwa katika ajira hatarishi.
Hayo yamesemwa na wadau mbalimbali wa kutetea watoto walioshiriki Kongamano la kujadili sera, sheria na miongozo ya kumlinda mtoto, wakiongozwa na Muungano wa Mashirika dhidi ya Utumikishwaji wa Watoto Tanzania (TCACL).
Akizungumzia na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mjumbe wa Bodi ya TCACL, Ibrahim Samata amesema kasi ya watoto kuajiriwa hasa kwenye kilimo ni kubwa na sababu kubwa ni umaskini wa familia.
“Ukitazama takwimu za Ofisi ya Takwimu Tanzania (NBS), Shirika la Chakula Duniani (FAO) na Shirika la Kuwahudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) kuna watoto takribani milioni 4 hadi 5 wapo kwenye ajira, hivyo sisi kama mashirika ya kutetea watoto tumeamua kukaa pamoja na kujadiliana namna ya kuwakomboa kisheria, kisera na miongozo,” amesema.
Samata amesema kwa mujibu wa taarifa mbalimbali kwa hapa nchini sekta ya kilimo hasa katika mikoa inayoongoza kuzalisha, ndio inatoa ajira kwa watoto na kwamba jitihada za pamoja zinahitajika.
Amesema taarifa zinaonesha sababu ya watoto kuajiriwa hasa kwenye kilimo ni umaskini unaokabili familia hasa za vijiji.
Mjumbe huyo wa bodi ameishauri serikali kuweka mkazo kwenye utekelezaji wa mipango madhubuti ya kuimarisha uwezo wa kaya, hali ambayo itapunguza umaskini na watoto kuepukana na ajira.
Naye Kaimu Mwenyekiti na Mjumbe wa Bodi ya TCACL, Wakili Edna Kamaleki, ameiomba serikali kuangalia upya sheria ya mtoto, ili kuepusha mgongano ambao unatokea kisheria.
Amesema TCACL imeweza kukuwa kwa kasi kubwa ambapo kwa sasa wana wanachama zaidi ya 50, hali ambayo inasaidia mapambano dhidi ya ajira kwa watoto kufaniwa kwa urahisi.
Kwa upande wake Mtaribu wa TCACL, Scolastica Pembe amesema utafiti waliofanya umebaini kuwa wazazi wote wawili ni muhimu katika malezi ya watoto, hali ambayo iwezesha watoto kutojihusisha na ajira mapema.
“Malezi ya watoto yanahitaji ushiriki wa baba na mama kwa asilimia kubwa, hivyo nichukue nafasi hii kuwashauri wazazi wenzangu kulinda watoto ili wasijihusishe na matukio mabaya ikiwemo ajira mbaya,” amesema.
Mtaribu huyo amesema katika kumlinda mtoto ni vema sheria zinazomhusu mtoto ziangaliwe upya kwani zina mkanganyiko ambao kwa upande fulani ni changamoto kwa mtoto.
Pembe amesema Sheria ya Ndoa inaruhusu mtu kuolewa akiwa na miaka 14, Sheria ya Ajira itambua kuwa mtu anaweza kuolewa akiwa na miaka 14, wakati huo huo Sheria inasema mtoto ni yule aliye chini ya miaka 18, hivyo mkanganyiko huo unatakiwa kupatiwa majibu sahihi.
Mkurungezi Mkuu wa Mtandao wa UN Global Compact Tanzania, Masha Macatta Yambi, amesema takwimu za dunia zinaonesha takribani watoto milioni 200 wanatumikishwa katika maeneo mbalimbali na kwamba milioni 120 wanafanya kazi katika mazingira hatarishi, huku milioni 73 wakiwa chini ya miaka 10.
Yambi amesema sekta ya kilimo na madini ndio inatoa ajira kwa asilimia kubwa kwa watoto, huku Ukanda wa Kusini mwa Afrika, ikiwemo Tanzania ndio unaongoza.
“Mazao ya biashara kama chai, mwani, miwa, tumbaku, karafuu, mkonge na mengine, ndio yanachangia ajira kwa watoto, hivyo inawezekana tunafurahi kupata mapato, ila tunaua kizazi cha baadae, kwani kinakosa elimu. Hali kama hiyo ipo kwenye madini, lazima tubadilike,” amesema.
Mkurugenzi huyo amesema sekta binafsi ni moja ya sababu kuu ya watoto kuajiriwa, hiyo ikitokana na kutaka kulipa kidogo ili wapate faida kubwa.
Mwakilishi Mkazi wa UNICEF Tanzania, Elke Wisch amesema ofisi yake itashirikiana na wadau wote ambao wanapigania za watoto, kwani watoto ni nguzo muhimu kwa dunia.
“Sisi UNICEF tunathamini sana watoto, hivyo tunaipongeza serikali ya Tanzania kuendelea kurekebisha na kusimamia sheria zanazomlinda mtoto, tutaendelea kushirikiana na wadau wote, ili mtoto awe salama,” amesema.
Akifungua kongamano hilo, Waziri wa Sheria na Katiba, Balozi Dk Pindi Chana amesema serikali imejipanga vizuri kuhakukisha watoto wanakuwa salama kisheria na kisera.
Dk Chana amesema katika kufanikisha hilo wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Mambo ya Ndani na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa watakutana na kujadiliana kuhusu eneo hilo.
Amesema serikali haitasita kuchukua hatua kwa mtu au taasisi yoyote ambayo itabainika kumtumikisha mtoto kinyume na sheria.
Waziri Chana amewataka wadau wa TCACL kuwasilisha mapendekezo na maoni yao kuhusu namna ya kukabiliana na ajira kwa watoto na kwamba serikali itayafanyia kazi.
Hakuna maoni: