Na Mwandishi Wetu,
Arusha.
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), umesema upo katika hatua za mwisho za kuondoa kaya 400,000 ambazo zilikuwa kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini baada ya kuweza kuboreka kimaisha.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Shadrack Mziray amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao wamefanya ziara ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na TASAF mkoani Arusha.
Alisema tangu mfuko huo uanzishwe umeweza kusajili zaidi ya kaya milioni 1.3 zenye wanufaika zaidi ya milioni 5.2, hivyo baada ya kufanya tathmini wamebaini kaya laki nne zinapaswa kuhitimu kunufaika na mpango.
"TASAF ipo kwa zaidi ya miaka 24 sasa tumeweza kufikia kaya maskini milioni 1.3 zenye wanufaika milioni 5.2, baada ya kuchakata tumebaini kaya laki nne zimeboreka kimaisha hivyo hazina sifa ya kuendelea na mpango huu," alisema.
Mziray alisema mkakati huo wa kuondoa kaya laki nne haujaungwa mkono na wahusika pamoja na baadhi ya wanasiasa, lakini hakuna namna kwani kutowaondoa kuwakwamisha malengo ya mfuko.
Alizitaka kaya ambazo zitaguswa na uamuzi huo zitambue kuwa mfuko huo unapaswa kuwakomboa Watanzania asilimia 26 wanaoishi katika umaskini.
Mziray alisema hadi sasa mfuko umegusa asilimia 8 ya maskini nchini, hivyo mikakati yake ni kuhakikisha inafikia asilimia 26 iliyopo.
Alisema iwapo uamuzi huo utaungwa mkono na wa wadau wote utasaidia kufanikisha mipango yao.
Mkurugenzi huyo alisema mfuko huo ulianza kwa kutekeleza miradi ya miundombinu ya afya, elimu na maji ambapo halmashauri 42 za Tanzania Bara na Zanzibar ila kwa sasa wapo katika halmshauri zote 186.
“Tanzania kuna umaskini wa mahitaji ya msingi ambapo takwimu zinaonesha ni asilimia 26 ya Watanzania wote na umaskini wa kukosa hata mlo mmoja ni asilimia 8. Hivyo mkakati wetu TASAF ni kuhakikisha hizi asilimia zinaisha kwa kushirikiana na jamii husika,” alisema.
Aidha, Mziray alisema TASAF inatarajia kutumia Sh trilioni 2 kwa ajili ya mpango wa pili ulioanza 2020 hadi 2025 na kuzitaka jamii zitakazo nufaika kutunza na kulinda miradi husika.
“Hapa Arusha tumetekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu kupitia ufadhili wa OPEC, lakini tunashukuru ushiriki wa wananchi ni mkubwa sana,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi TASAF, John Steven alisema mfuko huo umewezesha asilimia 97.6 ya watoto wa kaya za maskini kupata huduma za kliniki na asilimia 98.3 kusoma shule.
Steven alisema pia TASAF imenufaisha kaya 24,000 zenye watu wenye ulemavu katika kaya milioni 1.3 ambazo wamezitambua na kuzisajili.
Steven alisema TASAF imefikia zaidi ya wananchi milioni 5.2 katika halmashauri za wilaya, miji na majiji 186 ambapo wanawake ni asilimia 55.7 na wanaume asilimia 44.3.
Alisema mfuko huo umeweza kubadilisha maisha ya kaya mbalimbali, hali ambayo inatoa msukumo wa kuendelea na miradi ambayo inatekelezwa.
Mkurugenzi huo alisema takwimu zinaonesha walengwa wamenufaika na huduma za kijamii ikiwemo afya na elimu, hali ambayo inatoa tafsiri kuwa mradi huo unalipa.
“TASAF imeweza kuleta mabadiliko katika sekta mbalimbali, lakini kubwa zaidi ni sekta ya elimu na afya ambapo tumeona asilimia 97.6 ya walengwa wameweza kupata huduma za afya na asilimia 98.3 waneweza kusoma.
Ila kubwa zaidi ni watoto 4,600 kutoka familia maskini wamefanikiwa kujiunga na elimu ya juu katika vyou mbalimbali na kufanikiwa kupata mkopo kwa asilimia 100,” alisema.
Alisema kupitia TASAF walengwa wamekuwa wakipata ahueni katika baadhi ya huduma zinazotolewa kwenye huduma za afya na elimu.
Mkurugenzi huyo alisema mchakato wa kuwapata wanufaika wa TASAF unahusisha wananchi wenyewe kwa kuchagua nani apate.
Steven alisema katika eneo la ukuzaji uchumi wa kaya maskini kwa miaka 24 TASAF imeweza kusajili vikundi 60,327 vyenye walengwa zaidi laki nane wameweza kuweka akiba Sh bilioni 7.9 na kukopeshanya zaidi ya Sh bilioni 3.2.
Pia alisema program hiyo imewezesha wananchi kupata ajira za muda, hali ambayo inakuza uchumi wa wananchi na nchi kwa ujumla.
Alisema awamu ya pili ya program hiyo miradi 37, 331 imetekelezwa katika halmashauri 123 na kwamba wanarajia kufikia halmashauri 65 zilizobakia.
Mwenyekiti wa kijiji cha Oldonyowas wilayani Arusha, mkoani humo, Godfrey Ayo alisema TASAF imewezesha kijiji hicho kuwa na shule ya Sekondari Oldonyowas hali ambayo imechochea watoto wengi kusoma.
Diwani wa kata ya Bwawani, Justine Saray ameipongeza Serikali kupitia TASAF kwa kuwajenga hospitali kwenye kijiji cha Temi ya Simba ambayo itapunguza vifo vya mama wajawazito na watoto.
Hakuna maoni: