TMDA YAKANUSHA UWEPO PARACETAMOL INAYOBABUA NGOZI.

 


Na Mwandishi Wetu.

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imekanusha uwepo wa Dawa ya Paracetamol inayodaiwa kubabua ngozi.


Kwa mujibu wa taarifa liyotolewa kwa umma na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo, imesema taarifa iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uwepo wa dawa hiyo, haina ukweli na kuwataka wananchi waipuuzie.


Akinukuu taarifa hiyo Dk Fimbo amesema hadi sasa wao kama makala hawajatambua dawa hiyo na kuwataka wananchi kusambaza taarifa za uongo ambazo zinaleta taharuki.


"Dawa hiyo inadaiwa kuwa ni paracetamol mpya nyeupe sana na inayong'aa, madaktari wanashauri kuwa ina virusi vya "Machupo", inayochukuliwa kuwa moja ya virusi hatari zaidi ulimwenguni na kiwango cha juu cha vifo.


Aidha, mtoa taarifa anaitaka jamii kuisambaza taarifa hiyo kwa kila mtu aliyeko katika orodha yake ya mawasiliano ili kuokoa maisha.


Anamalizia kwa kusema ‘’Nimefanya 

sehemu yangu, sasa ni zamu yako. Kumbuka kwamba Mungu huwasaidia wale wanaosaidia wengine. ‘’Sambaza kama ilivyopokelewa’’.


Dkt.Fimbo ameeleza kuwa, taarifa hiyo imekuwa ikijirudia mara kwa mara na TMDA imekuwa ikitolea ufafanuzi

ikiwemo taarifa ya mnamo tarehe 10 Mei, 2023, juu ya dawa aina ya P-500® 

(PARACETAMOL) ya Apex Laboratories Private Limited, Tamil Nadu, India 

iliyodaiwa kuwa na virusi hivyo.


"TMDA inapenda kuufahamisha umma kwa mara nyingine kwamba hakuna virusi vinavyojulikana kwa jina la Machupo. Aidha, virusi vya aina yoyote haviwezi kuishi kwenye kidonge. 


Dawa zenye kiambata hai cha paracetamol inayotumika kutibu homa na maumivu zilizopo katika soko nchini kwa majina mbalimbali ya kibiashara zimesajiliwa baada ya kuthibitishwa kuwa zinakidhi vigezo vya usalama, ubora na ufanisi unaotakiwa na 

hivyo, ni salama kwa matumizi yaliyoainishwa," ameongeza. 


Katika hatua hiyo, TMDA inapenda kuwahakishia wananchi kuwa inaendelea kutimiza wajibu wake wa 

kulinda afya ya Jamii kwa kuhakikisha kuwa bidhaa tiba zinazotumika nchini ni zile zenye kukidhi matakwa ya ubora, usalama na ufanisi.


Vilevile, mamlaka inapenda kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kupata ufafanuzi kutoka kwenye mamlaka husika kabla ya kusambaza taarifa zinazoweza kuleta taharuki kwenye Jamii.


TMDA ndio yenye jukumu la kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa tiba nchini ambapo ili kuhakikisha kuwa bidhaa tiba (zikiwemo dawa) zilizoko katika soko nchini zinakidhi matakwa ya usalama, ubora na ufanisi, TMDA imeweka mifumo mbalimbali 

ya udhibiti ikiwa ni pamoja na tathmini na usajili, ukaguzi, uchunguzi wa kimaabara na ufuatiliaji wa ubora na usalama wa bidhaa katika soko. 


Aidha, amesema wananchi wanaweza kupiga simu ya bila malipo: 0800110084 endapo wapatapo taarifa za mashaka kama hizo.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.