Na Mwandishi wetu,
Dar es salaam.
WANANCHI mbalimbali wamejitokeza kupata elimu kuhusu aina ya miamba na namna ya kupima sampuli za madini ya Metallic kwenye mashine ya XRF kwenye Banda la Tume ya Madini katika maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam ‘Sabasaba’
Mashine hiyo ni maalum inayotumika kupima madini ya metallic kwa njia ya MIONZI /X-RAY na kisha kutoa majibu kwa kuonyesha madini hayo yaliyopimwa yana mchanganyiko wa madini gani, pamoja na madini yote yaliyomo ndani ya metali hiyo kwa asilimia tofauti tofauti.
Akitoa elimu hiyo kwa wananchi, Afisa Maabara kutoka Tume ya Madini, Zuwena Mtoo amesema Madini yapo ya aina nyingi duniani lakini huwa hayakai yenyewe, lazima yanakuwa yamechanganyikana na aina mbalimbali nyingine za madini katika miamba
Amesema, watu wanaonunua dhahabu ambao wanaogopa kutapeliwa kwa kuuziwa dhahabu feki wafike kwenye banda la Tume ya Madini kupata elimu ya namna ya kutambua miamba na madini mbalimbali pia wanaweza kupima Hereni, Mikufu ya Dhahabu na Silva katika banda na kushauri wananchi kuitumia fursa hii kufika katika Maabara ya Tume ya Madini iliyopo Msasani jijini Dar es Salaam ili kubaini aina ya miamba.
" Hii mashine ina kioo maalum itakuonyesha kwenye kioo madini yaliyomo ndani mfano ukipima dhahabu baada ya mionzi kuscan itakuonyesha dhahabu ipo asilimia 11 na Silver ipo asilimia 89 sasa wewe ukiona hivi unajua moja kwa moja ulichouziwa ni feki ama si feki," amesema Zuwena.
Amesema pia kuna mashine ya kupima sampuli za miamba kwa njia ya mionzi ambayo inatoa majibu ya ‘elements’ zote zilizomo kwenye huo mwamba na majina yake na wingi wake kwa kukuwekea asilimia yaani kama ni shaba utaona itaandika "CU"....%, kama ni madini ya chuma itaandika "Fe"....% kama ni dhahabu ipo itaandika "Au"....%.
Aidha, Zuwena ametoa wito kwa wananchi wanaokuja kwenye maonesho ya Sabasaba kutembelea banda la Tume ya Madini ili pia kujionea madini ya vito mbalimbali na kujifunza fursa zilizopo katika Sekta ya Madini.
Kauli mbiu ya mwaka 2024 katika Maonesho ya Sabasaba ni ‘Tanzania Mahali Sahihi pa Biashara na Uwekezaji’.
Hakuna maoni: