Na Selemani Msuya,
Kilimanjaro.
ZAIDI ya walengwa 690 waliopo kwenye Mradi wa Mpangp wa Kunusuru Kaya Masikini unaratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Halmashauri ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wamesema wapo tayari kupungwa katika mpango huo.
Mwandishi wa habari hii ameini hayo wakati akizungumza na walengwa hao kutoka mtaa ya Relini kata ya Bomambuzi, Kilimani kata ya Kaloleni na kwingineko ambapo walipongeza TASAF kwa kuwawezesha na kwamba kwa sasa wapo tayari kupambana bila msaada wa mfuko huo.
Valeria Teti mama wa miaka 56 mkazi wa mtaa wa Relini kata ya Boma Mbuzi, amesema kwa hatua ambayo amefikia yupo tayari kutolewa ili kuachia wananchi wengine wenye hali mbaya kimaisha nao wanufaike.
Amesema TASAF imemtoa katika dimbwi la umaskini ambapo kwa miaka takribani tisa ya kupata msaada ameweza kuandika historia mpya kwenye maisha yake na kuwataka walengwa wapya kuzingatia nidhamu ili kuweza kunufaika.
“Mimi nimeingia TASAF mwaka 2014, walinikuta naishi katika nyumba mbovu, nakula mlo mmoja, kusema kweli hali yangu ilikuwa mbaya, ila kwa sasa nimejenga nyumba yangu nzuri, nimewka umeme, nina televisheni na kusema kweli naweza kukidhi mahitaji ya familia yangu na kushiriki katika mambo ya kijami, nipo tayari kutoka, ili wengine waingie,” amesema.
Valeria amesema pia kupitia TASAF ameweza kusomesha watoto wake, kukata bima ya afya na kupata mavazi, hivyo anajiona mtu wa kipekee katika maisha yake kwa sasa.
"Ninafuraha sana TASAF wamebadilisha sana maisha yangu baada kunufaika na mpango wa kunusu kaya masikini, hamuwezi kuamini niliaza kwa kupika maandazi na nilikuwa naishi kwenye nyumba ya ndogo. Nilitelekezwa na familia ila TASAF ikanikomboa nashukuru sana, kwani nimefanya makubwa na ninaendelea,” amesema.
Mwana mama huyo amesma kwa manufaa hayo anapata nguvu ya kukubaliana na maamuzi ya TASAF, huku akiwataka walengwa wengine kukubalina na hali hiyo ili wengine waweze kuingia kwenye mpango.
Kwa upande wake Federika Swai mkazi wa Njoro Viwandani, amesema alianza kupokea shilingi 60,000 ambapo kwa hatua ambayo amefikia yupo tayari kutoka TASAF, kwani kwa asilimia kubwa ameweza kutimiza malengo yake.
“Kabla ya kuingia TASAF maisha yake yalikuwa magumu hadi ilifikia hatua ya kukata tamaa kabisa hali iliyokuwa inamfanya kufikiria mambo mengi sana lakini baada ya kupata uwezeshwaji na mafunzo na kuazia kufanya shughuguli za ufugaji maisha yaliaza kubadilika, kwangu mfuko huu umenikomboa,” amesema.
Amesema TASAF imemuwezesha kufanya shughuli za ufugaji wa mifugo mbalimbali ambapo ana Ng'ombe wawili, Mbuzi wanne, Kuku 20, Sungura nane na Bata wanne, na kupeleka watoto wawili Chuo Kikuu Dar es Salaam, kwakifupi maisha yake yamebadilika.
“Nashukuru sana TASAF kwa kweli awali nilikuwa nimechoka sana na sikuwa hivi ninavyoonekana nilikuwa hali mbaya nilikuwa naishi kwenye nyumba kaudongo lakini kwa sasa nipo kwenye mpango wa kujenga nuumba ya kisasa, watoto wanasoma, uhakika wa kula upo na mambo yanaenda na hata nikisema nipishe wenzangu kwenye mpango huu nipo tayari kwani naweza kupambana mwenyewe,” amesema Fedirika.
Naye Sarah Shengwatu mkazi wa Kaloleni ambaye ni fundi cherehani amesema TASAF imeweza kumuongozea kipato ambapo ameweza kufungua ofisi ya kushonea nguo na kwamba yupo tayari kutoka kwenye mpango.
Sara amesema awali alikuwa hana mashine ya kushonea, ila TASAF ilimfanya aweze kuwekeza kidogo kidogo na sasa anamiliki mashine yake mwenyewe na maisha yameboreka.
“Nilikuwa napokea Shlingi 44,000 ambapo nimeweza kuhudumia familia na kuwekeza kidogo kidogo na sasa nipo hapa ambapo nimefikia, kusema kwenye nawapongeza TASAF na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imejalia kubadilisha maisha yangu,” amesema.
Sara mwenye miaka 47 amesema kabla ya TASAF walikuwa wanapata mlo mmoja kwa siku ila kiuhalisia sasa mambo yamebadilika na kwamba alipofikia anaweza kuendelea mwenyewe.
Amesema awali shughuli zake za kushona alikuwa anafanyia nyumbani lakini kutokana na kunufaika na TASAF hivi analipa kodi.
“Ninawatoto watatu lakini namshukuru Mungu sasa wanasoma, wanauhakika wa kula na mambo mengine yanaendelea ukilinganisha na nilikotoka. Kwa kifupi sikuwa hivi lakini sasa ninafanya shughuli yangu hii japo hapa nilipohamia bado sijafahamika Sana lakini mambo yanakwenda ."Amesema Sarah .
Shufaa Mfinanga mkazi wa mtaa wa kilimani ambaye anajishughulisha na biashara ya genge la bidhaa mbalimbali amesema TASAF imeweza kufanya mapinduzi makubwa kwenye maisha yake na hapo alipo yupo tayari kujiendeleza mwenyewe.
Amesema kupitia TASAF wamedhamiria kupitia Kikundi chao la Lukundo kujengeana nyumba ili kuondoka na na nyumba za kupanga.
“Mungu ambariki sana Rais Samia kwa kazi nzuri na kubwa anayoifanya, nahakikisha kuwa sitamuangusha. Nina genge hili kama mnavyoona niliaza kidogo kidogo sasa linakuwa wateja wanakuja mambo ni mazuri, nipo na baba yangu mzazi namhudumia, watoto wanasoma uhakika upo kwa kweli nawashukuru sana waratibu wetu kutoka Manispaa ya Moshi,” amesema.
Naye Hamad Masumbuko miaka 27, mkazi wa mtaa wa Kilimani kata ya Kaloleni ambaye ni mlemavu amesema amejiunga TASAF Januari mwaka jana ambapo kwa sasa anaona maisha yake yamekuwa yenye neema.
“Mimi kama mnavyoniona hapa ni mlemavu, lakini nimefungua duka la kuuza mitungi ya gesi, kusema kweli maisha yangu yamebadilika sana na imani yangu siku chache zijazo nitakuwa nimepiga hatua kubwa,” amesema.
Amesema ameingia TASAF kupitia mgongo wa wazazi wake, hivyo ameamua kupambana kupitia msada huo ili siku moja awe anaishi na familia yake, hivyo amemuomba Rais Samia kuhakikisha anaongeza nguvu kwenye kundi hilo, akiwemo yeye.
Hamad amesema biashara hiyo imekuwa ikimpatia faida na wakati mwingine hasara, hivyo ameomba aongezewe mtaji ili kukua kibiashara.
“Mwanzoni mwa mwaka huu TASAF ilinipatia Sh 350,000 ambazo zimeweza kuniongezea nguvu kwenye biashara yangu, hivyo sijakata tamaa na kama wataona mimi nafaa kutolewa kwenye mpango nitakubali, pamoja na ukweli kuwa bado nawahitaji,” amesema.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Lukondo mtaa wa Kilimani kata ya Kaloleni, Fatuma Kimaro miaka 47 amesema TASAF imeweza kuwakomboa wananchi wengi saha wakina mama, hivyo ameuomba mfuko huo kuweka mkazo katika kundi hilo ambalo linapitia katika mazingira magumu.
“Mimi na wenzangu wa Kikundi cha Lukundo tumenufaika, mfano mimi nimeweza kulea watoto wangu wanne kwa kuwa ni mjane, na nunua mikungu 10 hadi 15 kutoka mikungu mitatu, na nimekuwa nikipokea Shilingi 67,000, ila walipunguza kulingana na majukumu kupungua. Ila hivi karibuni nilipewa Shilingi 350,000 ambayo imesaidia kuongeza mtaji,” amesema.
Amesema wamekubalina kujengeana nyumba kwa kila mwana kikundi na kwamba ujasiri huo unasababishwa na TASAF. “Tupo 12 ambapo kila wiki tunanunua hisa na tupo tayari kutoka kwenye mfuko,” amesema.
Hakuna maoni: