BRELA YAKUSANYA MAONI KUTOKA KWA WADAU KUHUSU RASIMU YA MKTABA WA WIPO WA ULINZI WA MAUMBO BUNIFU.






DAR ES SALAAM.

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) wamekutana na wadau, Septemba 5, 2024, jijini Dar es Salaam, kujadili rasimu ya Mkataba wa Sheria ya Kimataifa kuhusu Ulinzi wa Maumbo Bunifu na Michoro. Kikao hicho kilikuwa na lengo la kupata maoni na ushauri wa wadau kuhusu mkataba huo.


Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, aliwahimiza wasanifu majengo na wajasiriamali kuongeza ubunifu katika maumbo na vifungashio vya bidhaa zao ili kuongeza thamani na ushindani kitaifa na kimataifa. Nyaisa alieleza kuwa maoni yatakayokusanywa yatatumika kwenye mkutano wa kideplomasia wa Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (WIPO) utakaofanyika Riyadh, Saudi Arabia, kuanzia Novemba 11 hadi 22 mwaka huu.


Mkataba huo wa WIPO unalenga kuweka mfumo wa kimataifa wa usajili na ulinzi wa maumbo bunifu. Mfumo huu utawezesha maombi ya ulinzi wa bunifu kuwasilishwa kupitia WIPO na kupata ulinzi katika nchi nyingi kwa wakati mmoja, kupunguza gharama na ugumu wa usajili. Nyaisa alisema kuwa endapo sheria hiyo itapitishwa na Tanzania, itatoa fursa kwa wabunifu wa Kitanzania kusajili na kulinda kazi zao kimataifa, hivyo kuongeza ushindani wa bidhaa zao.


BRELA pia imesema itatoa elimu zaidi kwa wajasiriamali na wabunifu kupitia ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Shirika la Miliki Kanda ya Afrika (ARIPO), ili kuongeza uelewa na usimamizi wa miliki bunifu. Mustafa Haji kutoka BPRA alitaka vikao vya namna hii pia kufanyika Zanzibar kwa manufaa ya kitaifa, wakati Dkt. Perfect Melkiori kutoka UDSM alisisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa wanafunzi na wafanyakazi kuhusu thamani ya bunifu ili kuepuka udanganyifu wa kuuza kwa bei ndogo.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.