MKUTANO WA 11 WA MERCK FOUNDATION KUFANYIKA TANZANIA






DAR ES SALAAM.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, ametangaza kuwa Taasisi ya Merck Foundation itafanya mkutano wake wa 11 nchini Tanzania tarehe 29 na 30 Oktoba 2024, jijini Dar es Salaam. 


Akizungumza na waandishi wa habari mnamo Septemba 18, 2024, Waziri Gwajima alisema kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, atakuwa mwenyekiti wa mkutano huo. Ni mara ya kwanza mkutano huu unafanyika nchini Tanzania, baada ya Rais Samia kuridhia ombi la Taasisi hiyo.


Waziri Gwajima alisisitiza kwamba mkutano huu unalenga kuonyesha jitihada za Serikali za kuwekeza katika sekta ya afya, hasa afya ya akina mama na watoto, na kwamba unaleta fursa ya kuimarisha utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya kimataifa.


Mkutano huo utaandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Taasisi ya Merck Foundation, ukitarajiwa kuhudhuriwa na wenza wa marais kutoka nchi 22 za Afrika, ambapo Mwenza wa Rais wa Zanzibar, Mariam Mwinyi, atawakilisha.


Aidha, mkutano utajumuisha mawaziri wa afya, jinsia, mawasiliano, elimu, na ustawi wa jamii kutoka nchi zilizowakilishwa, pamoja na wataalam wa huduma za afya, wasomi, na waandishi wa habari. Jumla ya washiriki wapatao 500 wanatarajiwa kushiriki, wakiwemo wale watakaoshiriki kwa njia ya mtandao.


Mkutano utajadili mada muhimu, ikiwa ni pamoja na afya ya mama na mtoto, saratani, kisukari, na shinikizo la damu. Aidha, kutakuwa na mafunzo kwa vyombo vya habari kuhusu mipango ya maendeleo na jinsi ya kuimarisha uwezo wa upatikanaji wa huduma za uzazi salama barani Afrika.


Waziri Gwajima alitoa wito kwa Watanzania kudumisha amani na umoja ili kuwaleta wadau mbalimbali wanaofika nchini kwa ajili ya mikutano na shughuli za utalii. Mkutano huu unatarajiwa kuwa jukwaa la kubadilishana maarifa na uzoefu kuhusu masuala mbalimbali ya afya, na kutoa fursa ya kujadili changamoto zinazokabili jamii katika sekta ya afya.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.