EACOP: TUNAHESHIMU NA KUTHAMINI MILA,TAMADUNI NA DESTURI ZA MAKUNDI YA KIASILI KATIKA MRADI WETU

 


Na Florid Mapunda

Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP) unahusika na usafirishaji wa mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga kabla ya kusafirishwa nje ya nchi kwa ajili ya masoko ya kimataifa. 

Katika utekelezaji wake, mradi huu wa EACOP wakati wote unaheshimu mila na desturi za watu wanaoishi au kupitiwa na mradi huu, wakiwemo wale wa mila za asili (Indigenous People) ambao wanatambulika katika jamii.


Katika kuhakikisha mila na tamaduni zao zinaheshimiwa, EACOP ilifanya tathmini ya kina juu ya haki za jamii hizi athari na kuangalia mchakato wa upatikanaji wa ardhi, ili kutambua maeneo ya makundi ya kikabila ya watu wa asili ambao wanaguswa moja kwa moja na mradi huu. 

Hivyo, makundi manne yalibainishwa ambayo ni Wamaasai, Wadatoga (Taturu na Barbaig) na Wakiye.


Meneja Mkuu wa EACOP nchini Tanzania, Wendy Brown, alieleza kuwa baada ya utambuzi kukamilika, mradi uliheshimu mila na tamaduni za makundi haya na kuridhia utekelezaji wake katika maeneo yao.


 “Walifurahi na kushirikiana na EACOP kikamilifu kwa sababu tunathamini utamaduni na desturi zao,”


“Tulifurahi na kuwashukuru kwa ushirikiano wao. Walitambua kwamba tunathamini sana utamaduni na desturi za makabila yao,” alisema Bi. Brown.


Katika utekelezaji wa mradi mkubwa kama EACOP, Bi. Brown alieleza kuwa kuna athari zinazoweza kutokea katika jamii.


Ili kuhakikisha jamii hizi tamadunia na mila zao zinaheshimiwa, timu ya maafisa wa EACOP imekuwa ikikutana na jamii hizi na viongozi wao wa jadi kwa muda wa miaka kadhaa mara kwa mara ili kuwashirikisha na kuheshimu maamuzi yao. 


Lengo ni kufikia makubaliano kuhusu mchakato wa kuhusisha jamii, kuwajenga uwezo wao na kusimamia athari zinazotokea katika utekelezaji wa mradi huu katika maeneo yao ya kijadi na kiasili.


“Mradi umedhamiria kuheshimu mila na desturi za makundi haya,”


“Hivyo, tunajitolea kuhakikisha usimamizi mzuri wa athari zozote zinazohusiana na desturi zao,” alifafanua Mkuu wa kitengo cha Habari na Mawasiliano wa EACOP (Tanzania), Bi. Catherine Mbatia.


Katika kuhakikisha hili linafanyika kwa ukamilifu, alisema kuwa EACOP imesaini makubaliano kadhaa na jamii zinazohusika zikiwemo za watu wa asili ikiwemo mikataba miwili ya Free, Prior and Informed Consent (FPIC).


Ujenzi wa bomba hilo la mafuta ghafi litakalofukiwa chini ya ardhi kwa ajili ya usafirishaji lina urefu wa kilomita 1,147 nchini Tanzania, likipita kupitia Mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.  

Kwa upande wa Uganda, ujenzi wa bomba hilo unahusisha kilomita 296 pekee.


Bi. Mbatia alieleza kwamba katika kutekeleza miradi mikubwa kama hii inayovuta umakini wa kitaifa, kikanda na kimataifa, ni muhimu kuzingatia mikataba ambayo mradi wa EACOP unaingia na jamii husika.


Hii, anasema ni katika kuheshimu mikataba ya kimataifa inayotaka haki za watu ikiwemo wale wa asili zinaheshimiwa pale inapotokea asili, urithi, rasilimali na tamaduni zao kuguswa.


EACOP na viongozi wa jadi wa Jumuiya ya Wakiye walisaini makubaliano ya kwanza ya (FPIC) katika kijiji cha Napilikunya katikati ya mwaka 2022. 

Kama sehemu ya makubaliano haya, Bi Mbatia alielezea namna mradi ulivyokubaliana na jamii husika katika kuhamisha maeneo yao ya kitamaduni kutoka kwenye mti wa Baobab kwenye ardhi ya familia ya Lembulu hadi kwenye mti wa Baobab kwenye ardhi ya familia ya Oring’idi, mbali na Njia ya Bomba.


Hafla ya makubaliano hayo ilihudhiriwa pia na Bi Wendy na viongozi wa jamii ya Wakiye, wakiwemo mashahidi wa jamii ya Wakiye, NGOs zinazounga mkono jamii hiyo, Mshauri wa EACOP kuhusu Makundi ya Kikabila yanayojiita Watu wa Kiasili, na maafisa wa serikali ya wilaya ya Kiteto.


“Hili lilikuwa tukio kubwa la kijamii nchini Tanzania,”, alieleza Bi. Mbatia na kuongeza kuwa makubaliano haya katika kuheshimu mikataba ya kimataifa (FPIC) yalikuwa ni ya kwanza kabisa kusainiwa nchini Tanzania na ni miongoni mwa machache kupata kutokea barani Afrika.


Hivi Karibuni, EACOP ilisaini pia makubaliano ya pili ya FPIC na wanajumuiya wa Wataturu wanaoishi Mwamayoka katika Wilaya ya Igunga, Mkoa wa Tabora.


Kusainiwa kwa Makubaliano ya FPIC kuliuthibitishia jamii hiyo kwamba EACOP tayari ilichepusha njia itakayopitisha bomba ili kulinda makaburi yao ya asili na maeneo matakatifu kwa kuheshimu utamaduni na desturi zao.


Dk. Elifuraha Laltaika, Mshauri wa EACOP kuhusu Makundi ya Kikabila yanayojiita Watu wa Kiasili, amefafanua kuwa kupitia makubaliano haya, mradi wa EACOP umejizatiti kupunguza athari zinazohusiana na mradi.


“Najivunia sana Tanzania inajiunga na nchi chache katika kanda ambazo mikataba ya aina hii (FPIC) imesainiwa,”


“Hii inaonyesha kuheshimiwa kwa sheria ya kimataifa inayohitaji mila na tamaduni za jamii husika kuheshimiwa kabla na wakati wa utekeleza wa miradi.


“Hii ni hatua muhimu katika utekelezaji wa miradi ya aina hii barani Afrika,” alisema Dk. Laltaika na kuongeza: “Nimevutiwa sana namna mradi huu wa EACOP unavyoshirikiana na jamii za Wakiye na Wataturu na kuzishirikisha kufanya maamuzi yenye uelewa kuhusu haki zao.”


“Baada ya majadiliano yenye tija na jamii ya Taturu, anaendelea, “EACOP ilikubali pendekezo la jamii kuhusu kuchepusha njia ya bomba ili kuepuka kuathiri makaburi ambayo yana umuhimu wa kiroho na kitamaduni katika jamii hiyo. Hii ni alama ya mapenzi ya EACOP katika jamii hizi.” alisema Dk. Laltaika.


Kwa Dk. Laltaika, makubaliano ya FPIC na jamii ya Taturu yanaweka alama ya ushirikiano na kuonyesha thamani kubwa ambayo mradi wa EACOP imeionyesha kwa jamii hizi .


“Kipekee makubaliano haya ya FPIC yanaonyesha kuwa maamuzi ya jamii husika yameheshimiwa,”


“Hii ni nadra kwa sababu michakato mingi ya FPIC husababisha jamii husika kukubaliana na mradi na hii nadhani ni hatua ya kipekee inayostahili kupongezwa .”


Ameongeza “Tulihamasisha jamii hizi kuelewa na kuwezesha mchakato wote kabla ya sherehe za kusaini mbele ya wanajamii wote, wazee, na maafisa wa serikali.”


Dk. Laltaika anasema kuwa ushirikiano wa EACOP na jamii husika kupitia viongozi wa jadi ulianza mwaka 2017 na kufanyika kila robo mwaka.


Hii imepelekea kutambulika na kuheshimiwa kwa maeneo ya kiutamaduni na matakatifu yanayoweza kuathirika.


“Ushirikiano wetu umejikita katika kuhakikisha kwamba jamii za Wakiye na Wataturu zimearifiwa vizuri ili kufanya maamuzi sahihi kuhusu urithi wao wa kitamaduni na wa jadi,” anasisitiza Dk. Laltaika.


EACOP ina mikataba na mashirika (NGO’s) matatu yasiyo ya kiserikali yenye uzoefu katika kufanya kazi na jamii husika. 

NGOs hizo ni Ujamaa Community Resource Team (UCRT), Pastoralists Indigenous Non-Governmental Organization’s Forum (PINGO’s Forum) na Parakuiyo Pastoralists Indigenous Community Development Organisation (PAICODEO). 

Mikataba hii ilisainiwa kwa sababu nzuri. Kwanza, ili kukuza uwazi. Pili, ili mashirika yasiyo ya kiserikali kusaidia kuwasiliana na jamii za Makundi ya Kikabila yanayojiita Watu wa Kiasili, ili kusaidia kufafanua zaidi kuhusu mradi, michakato yake na athari zake na kuhakikisha kuelewa wa pamoja na kuruhusu jamii hizi kuiuliza EACOP maswali na kupatiwa majibu.


Akizungumza wakati wa kusaini Makubaliano ya FPIC wilayani Igunga, mwakilishi wa PINGO’s Forum, Nailejileji Tipop, aliushukuru mradi wa EACOP kwa kulinda maslahi ya Watu wa Kiasili na kuhifadhi utamaduni na desturi zao wakati wa utekelezaji wa mradi huu.


Pia aliushukuru mradi wa EACOP na Serikali kwa kutambua matakwa ya Watu wa Kiasili katika jamii.


Naye Mkuu wa jamii ya Wataturu, Gesuda Masanja pia aliushukuru mradi wa EACOP kwa kuheshimu tamaduni zao na kuchagua kubadilisha njia ya bomba ili kutoathiri makaburi ya mababu na viongozi wao wa jadi.


 “Mradi huu unaheshimu utamaduni na desturi za jamii ya Wataturu, na tunashukuru sana kwa hilo,” alisema .


Robert Mwagala, Afisa wa Wilaya ya Igunga (WEO), aliwashukuru watu wa jamii ya kiasili kwa kutoa ‘baraka’ za ujenzi wa mradi huu na kuidhinisha kupita kwa bomba hili la mafuta ghafi katika maeneo yao ya asili.


Godslove Kawiche, Afisa Utawala wa Igunga pia aliushukuru mradi wa EACOP kwa kuishirikisha jamii hiyo.


“Hatu hii inaonyesha ni kwa namna gani mradi huu upo karibu na jamii zinazopitiwa na mradi na kuheshimu mila na tamaduni zao. Huu ni mfano mzuri wa kuigwa,” alisema.


Mradi wa bomba hili pia unahusisha pia ufukiaji wa bomba lenye inchi 24 ardhini linalokinga joto, ujenzi wa vituo 6 vya kusukuma mafuta hayo, vituo vingine viwili vya kupunguza mgandamizo wa hewa na kituo cha baharini cha kusafirisha mafuta hayo nje ya nchi.


Baada ya Maamuzi ya Uwekezaji wa Mwisho (FID) ambayo yalifanyika tarehe 1 Februari 2022, East African Crude Oil Pipeline (EACOP) Ltd. tarehe 15 Februari ilikamilisha kuundwa kwa kampuni itakayosimamia ujenzi na uendeshaji wa bomba hili.


EACOP Ltd. ni kampuni inayoundwa na wanahisa wanne, ambapo TotalEnergies inamiliki hisa asilimia 62, huku mashirika ya kusimamia nishati ya mafuta nchini Tanzania (TPDC) na Uganda (UNOC) yakimiliki hisa asilimia 15 kila moja huku shirika la kusimamia nishati hiyo nchini China ( CNOOC ) likimiliki asilimia nane.


Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.