VIJANA 192 WA PROGRAMU YA JENGA KESHO ILIYO BORA WATUNUKIWA VYETI BAADA YA KUFUZU MAFUNZO YA MBOLEA.
DODOMA.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Bw. Joel Laurent amekabidhi vyeti vya mafunzo ya uendeshaji wa biashara ya mbolea kwa vijana 192 wa Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (Building a Better Tomorrow - BBT).
Ametoa vyeti hivyo tarehe 22 Septemba 2024, mara baada ya Vijana hao wa BBT kuhitimu mafunzo yaliyofanyika katika Shamba lao Chinangali ll Wilayani Chamwino Mkoa wa Dodoma ambapo vyeti hivyo vitawasaidia kujisajili kuwa mawakala wa pembejeo za mbolea.
Kwa kutambua umuhimu wa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Wizara ya Kilimo, TFRA imeratibu mafunzo hayo kwa kushirikiana na Idara ya Mafunzo ya Wizara ya Kilimo kupitia Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo (MATI) ili kutoa mafunzo ya uendeshaji wa biashara ya mbolea kwa kuzingatia Sheria ya Mbolea Na. 9 ya mwaka 2009.
Aidha, Mkurugenzi Laurent amesema matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka tani 500,000 kwa mwaka 2022/2023 hadi kufikia tani 840,000 Kwa mwaka 2023/2024 ongezeko hilo likichagizwa na ruzuku ya Mbolea inayotolewa na serikali ya Rais wa Jamhuri ya MUungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Ongezeko la matumizi ya mbolea nchini ni kubwa na TFRA inaendelea kupanua wigo wa utoaji elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima ili waendelee kunufaika na shughuli zao” Laurent aliongeza.
Amesema kila mwaka kiasi cha matumizi kinaongezeka na kukiri ongezeko hilo ni dalili nzuri inayoonesha kwamba wakulima wamebadilika kimtazamo na kuachana na kilimo cha mazoea kwenda kilimo cha kisasa kinachowawezesha kuongeza tija.
Hata hivyo amesema, Mamlaka inaendelea na kampeni yake ya Kilimo ni mbolea inayolenga zaidi katika kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea lengo likiwa kupata idadi kubwa ya watumiaji wa mbolea kwenye kilimo.
Amesema lengo la Mamlaka ni kuona kila mkulima anajua umuhimu wa mbolea na anazingatia matumizi sahihi ya mbolea kwenye kilimo wanachofanya.
Pamoja na hayo Laurent amesema, wakulima kutoka maeneo mbalimbali nchini wanazidi kujisajili kwenye mfumo,ili wapate mbolea ya ruzuku kwa ajili ya msimu wa kilimo.
Katika hatua nyingine aliwapongeza vijana wa BBT kutokana na mafunzo waliyopata,ambayo yatawajenga katika kilimo wanachoendelea kufanya.
Alisema mafunzo ya siku mbili yaliyotolewa kwao na yana maana kubwa katika maandalizi ya msimu wa unaoelekea kuanza hivi karibuni.
Pamoja na hayo Mkurugenzi wa TFRA,ameishukuru Wizara ya kilimo kutokana na kuwalea vizuri vijana wa BBT Jambo linalochangia kuzidi kukua kwa kilimo hapa nchini.
Naye Mratibu wa Mradi wa Jenga Kesho Iliyobora (BBT) Mathed Kahaya ameishukuru TFRA kwa mafunzo waliyotoa, huku akisema mafunzo hayo yasiishie hapo ili kuwakumbusha vijana hao mambo ya kuzingatia kwenye kilimo chao mara kwa mara.
Hakuna maoni: