WAMACHINGA KUFANYA MAREKEBISHO KATIBA YAO; MWENYEKITI AONGEZEWA MUDA.



Na Mwandishi Wetu,

Dar es Salaam.

Shirikisho la Umoja wa Machinga Tanzania (SHIUMA) limetangaza mpango wa kufanya marekebisho makubwa kwenye katiba yao, baada ya kugundua mapungufu yaliyopo. Kamati maalumu ya marekebisho imeundwa, ikijumuisha vyama 15 kutoka Tanzania Bara. Kamati hii inatarajia kuleta katiba bora itakayokidhi mahitaji ya shirikisho hilo.


Mwenyekiti wa Shirikisho hilo, Steven Lusinde, alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, akieleza kwamba marekebisho haya yanatokana na maelekezo kutoka kwa Msajili wa Jumuiya, ambaye alishauri kuboresha katiba kutokana na mahitaji ya sasa na ya baadaye. Lusinde aliongeza kwamba mwenyekiti atatembelea mikoa yote yenye migogoro ndani ya shirikisho hilo ili kutatua matatizo hayo, akilenga kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita katika kusaidia machinga.


Mwenyekiti pia alizungumzia kuhusu vitambulisho vya machinga, ambapo wamevipokea na kuvikubali. Hata hivyo, wametoa wito kwa serikali kupitia wizara husika kutoa elimu kwa machinga ili wawe na uelewa mzuri na kuwawezesha kununua vitambulisho hivyo bila kulazimishwa.


Kwa kuongeza, Lusinde alisema hivi karibuni wamekutana na kamishna wa TRA ili kujadili changamoto walizonazo na kuweka mikakati ya kulipa kodi kwa hiari, kuhakikisha taifa linapata mapato ya kutosha.


Lusinde alisisitiza kuwa wamachinga wanajipanga kuanzisha SACCOS yao wenyewe. Aidha, amewahimiza machinga wote kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura na kushiriki katika uchaguzi wa viongozi mbalimbali.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.