WANYAMAPORI WAKOROFI ZAIDI YA 200 WAUWAWA NA TAWA.

 









Na Mwandishi Wetu, 

Bagamoyo,Pwani.

ZAIDI ya wanyamapori 221 wameuwawa na Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) katika kipindi cha mwaka 2023/24 kutokana na kudhuru wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Hayo yamesemwa jana wilayani Bagamoyo mkoa Pwani na Ofisa Uhifadhi wa TAWA, Isaac Chamba wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari walioshiriki mafunzo ya siku mbili yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), kupitia Mradi wa Kupunguza Migongano Baina ya Binadamu na Viumbepori, chini ya ufadhilii wa Shiriki la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).

Chamba, amesema pamoja na kuuwa wananyapori 221 pia wamekuwa wakihamisha wengine zaidi ya 60 ili wasilete madhara kwa jamii inayozunguka hifadhi, mapori tengefu na maeneo mengine

Ofisa huyo amesema katika operesheni hiyo wamefanikiwa kuuwa viboko 63, fisi 43, nyati 27, simba 10 nyani na chui, huku wakifanikiwa kuhamisha simba 70, chui mmoja na fisi wawili.

Chamba amesema kwa mujibu wa sheria ya uhifadhi wa wanyamapori sura namba 283 kifungu cha 73 kinatoa mamlaka kwa afisa wa wanyamapori kuuwa mnyamapori yoyote ambaye anahatarisha maisha ya watu.

 “Maisha ya binadamu ni muhimu na tunayapa kipaombele kuliko maisha ya kiumbe yoyote yule anayeonekana anahatarisha maisha ya watu, lengo ni kuhakikisha jamii inakuwa salama na kuishi kwa amani” amesema Chamba.

Amesema kuwa TAWA inaendelea kuimarisha usalama kwa wananchi katika maeneo yote, huku akieleza kuwa mwaka 2023 idadi kubwa ya wanyamapori waharibifu waliouawa Kiboko pamoja na Mamba.

Chamba amesema wamekuwa wakichukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na changamoto wanyamapori waharibifu ikiwemo kufanya doria ya mwitikio wa haraka kwa kushirikiana na askari wa hifadhi, askari wa wanyamapori wa kijiji.

Amesema pia kwa miaka ya hivi karibuni wameweza kuwaondoa tembo zaidi ya 500 katika makazi ya watu na kuwarejesha katika hifadhi.

"TAWA imekuwa ikitekeleza majukumu yake ya kuhakikisha wanyamapori na wanadamu wanakuwa salama, hivyo katika kufanikisha hilo tumeweza kuuwa viumbepori 221 wakorofi, tumehamisha viumbepori zaidi ya 60 na mengine mengi," amesema.

Akizungumzia zoezi la kuwaondoa tembo amesema wilaya zilizohusika ni Nachingwea, Liwale, Bunda, Mwanga, Same, Mvomero pamoja na Mbarali.

Amebainisha kuwa changamoto iliyopo inatokana na uwepo wa shughuli za kilimo na mifugo katika maeneo ya mtawanyiko wa wanyamapori na kusababisha migongano baina ya wakulima na wanyamapori wanapokuwa wakipita katika maeneo hayo.

“Changamoto ni shughuli za kilimo hasa katika Wilaya ya Tunduru, Liwale, Nachingwea, Mvomero, Manjoni, Bunda, Serengeti ambazo zimekuwa na muongezeko wa matukio kutokana na shughuli za kibinadamu na matumizi ya wanyamapori katika maeneo hayo” amesema Chamba.

Amesema kuwa lengo ni kuhakikisha jamii inayoishi katika maeneo hayo inakuwa salama kwa kuendelea kufanya doria ya kudhibiti wanyamapori kwa kuwarejesha katika hifadhi.

Ameeleza kuwa wameendelea kutoa elimu ya hifadhi kwa jamii ikiwemo namna bora ya kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori kipindi wanapovamia katika makazi yao.

“Lengola elimu ni kuimarisha kuishi kwa pamoja kati ya binadamu na wanyamapori hususani katika maeneo yenye muingiliano wa matumizi ya ardhi baina ya binadamu na wanyamapori,” amesema Chamba.

Kwa upande wake mwenyekiti wa JET, Dk Ellen Otaru amesema chama hicho kimejipanga kutoa elimu kwa kundi la wanahabari ili kuhakikisha linatumia nafasi yake kuleta mabadiliko.

Otaru amesema iwapo waandishi wa habari watakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu migongano baina ya binadamu na wanyapori ni wazi kuwa suluhisho litapatikana.

Mkurugenzi Mkuu wa JET, John Chikomo amesema mradi huo unaotekelezwa na GIZ unahusisha Ukanda wa Ruvuma na Lindi katika Wilaya ya Liwale, Tunduru na Namtumbo.

Amesema JET imekuwa ikitumia waandishi kwenda na kuona kinachofanyika katika kukabiliana na migongano baina ya binadamu na wanyamapori na kwa asilimia kubwa kuna matokeo chanya.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.