SIKU YA MTOTO WA KIKE,ITUMIKE KUHAMASISHA WASICHANA KUSHIRIKI KIKAMILIFU KATIKA UCHAGUZI,KUGOMBEA NA KUPIGA KURA.
Dar Es Salaam
Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike tarehe 11 Oktoba 2024, mamlaka za serikali za mitaa zimesisitizwa kuhamasisha wasichana kushiriki katika uchaguzi kwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika ngazi za shule na jamii.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju, alitoa rai hiyo tarehe 2 Oktoba 2024 jijini Dar Es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari. Alisisitiza umuhimu wa watoto wa kike kujiandaa kuwa viongozi wa sasa na siku zijazo kupitia kushiriki kwenye chaguzi mbalimbali.
Mpanju alifafanua kwamba serikali inaratibu kuanzisha majukwaa maalum ya kuwajengea uwezo watoto shuleni, kwa msaada wa walimu, ili kukabiliana na vitendo vya ukatili vinavyowakabili watoto wa kike. Kati ya Septemba 2024, jumla ya madawati 3,618 yameundwa, ikiwa ni pamoja na 2,471 katika shule za msingi na 1,147 katika shule za sekondari.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni "Mtoto wa Kike na Uongozi; Tumshirikishe, Wakati ni Sasa", ikiwa na lengo la kuwasaidia wasichana kujifunza na kupata stadi za uongozi.
Kulingana na takwimu za Sensa ya Watu na Makazi za mwaka 2022, watoto wa kike nchini Tanzania ni milioni 14,680,895, lakini kundi hili linakabiliwa na changamoto kama vile vitendo vya ukatili, mimba za utotoni na ndoa za utotoni.
Taarifa ya Jeshi la Polisi kuhusiana na ukatili wa kijinsia inaonyesha kuongezeka kwa matukio ya ukatili dhidi ya watoto, ambapo mwaka 2023 kulikuwa na matukio 15,301, ikiwa ni ongezeko la asilimia 25.8 kutoka mwaka 2022. Mikoa yenye matukio mengi ni Arusha, Morogoro, na Tanga.
Mpanju aliongeza kuwa sababu za malezi duni ni pamoja na migogoro ya kifamilia, ambayo inachangia watoto kuingia kwenye ngono katika umri mdogo, na hivyo kupelekea mimba za utotoni.
Rebecca Gyumi kutoka taasisi ya Msichana Initiatives alithibitisha kuwa wadau wako tayari kuendeleza juhudi za kulinda mtoto wa kike kwa kushirikiana na serikali.
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike yanatambua changamoto za kipekee zinazowakabili wasichana, huku yakisisitiza umuhimu wa haki zao za msingi na ukuaji wao.
Hakuna maoni: