CCM IMESHINDA KWA KISHINDO UCHAGUZI SERIKA ZA MITAA KUTOKANA NA MAANDALIZI MAZURI NDANI YA CHAMA -CPA MAKALA.
Na Emmanuel Kawau,
Dar es salaam.
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimepata ushindi mkubwa wa asilimia 99.01 katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27, 2024, ambapo kimeshinda nafasi 12,150 za Uenyekiti wa Vijiji katika Vijiji vyote 12,271 vilivyoshiriki uchaguzi huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,CPA. Amosi Makala, amesema kuwa ushindi huo unaonesha imani kubwa ya wananchi kwa chama hicho, kwa uongozi thabiti katika kuleta maendeleo
"Chama cha Mapinduzi kinatumia fursa hii kuwashukuru Watanzania wote kwa kuendelea kukiamini na kukipa ushindi mkubwa. Ahadi yetu kwa Watanzania ni kwamba CCM itaendelea kuwatumikia kwa ufanisi na kwa weledi katika utekelezaji wa sera zake," alisema Makala.
Makala pia amevishukuru vyama vya upinzani kwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo, akieleza kuwa uchaguzi umefanyika kwa amani na demokrasia ya hali ya juu.
Pia Amesisitiza kuwa viongozi waliochaguliwa wanapaswa kufanya kazi kwa ufanisi, kuhakikisha wanawajibika kwa wananchi, na kusoma taarifa za mapato na matumizi ya mtaa. Aliongeza kuwa viongozi hawa wanapaswa kuepuka urasimu na kuwa na utendaji wa uaminifu wa hali ya juu.
Ushindi wa CCM, alisema Makala, umetokana na maandalizi mazuri na uratibu wa karibu uliofanywa na sekretarieti ya chama, ikiwa ni pamoja na ziara na kampeni zilizofanyika katika vijiji na vitongoji vyote nchini. Amesema kuwa migogoro ya vyama vya siasa, hasa ndani ya vyama vya upinzani, imechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha nguvu na mshikamano ndani ya CCM, na hivyo kusaidia katika kupata ushindi mkubwa.
Makala pia amekemea vikali matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea katika baadhi ya maeneo, akitaja matukio ya mauaji na majeruhi. Alisema kuwa CCM inalaani vitendo vya aina hiyo na kuwataka wanasiasa wote kuzingatia sheria na taratibu, na badala yake kujikita katika kushindana kwa hoja. "Viongozi wenzangu wa vyama vya siasa, tushindane kwa hoja na siyo kwa vurugu. Huu ni wakati wa kujenga nchi yetu, siyo kuharibu amani yetu," alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Makala amethibitisha kwamba CCM itaheshimu sheria na miongozo ya uchaguzi, na itaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi katika nyanja zote za maendeleo.

Hakuna maoni: