
DAR ES SALAAM.
Tamasha la pili la Samia Fashion Festival linatarajiwa kufanyika visiwani Zanzibar Jumamosi hii katika hoteli ya Golden Tulip. Tamasha hili la ubunifu wa mavazi linatarajiwa kuwa na uzito mkubwa na linabeba ujumbe wa kuenzi utamaduni wa Kitanzania na Kiafrika, huku likilenga kuwapa nafasi ya kuonyesha ubunifu wao vijana na watoto kutoka maeneo mbalimbali.Mwanzilishi wa tamasha hilo, Hadija Mwanamboka, alieleza kuwa lengo kuu la tamasha hili ni kuhamasisha na kuenzi sanaa ya mavazi ya Kitanzania, huku pia likilenga kusaidia watoto wanaoishi na VVU na kansa. Alisema kuwa mradi mpya unaohusisha watoto hao utakuwa na mchango mkubwa katika kutoa hamasa na kuelimisha jamii kuhusu changamoto wanazozipitia. "Tamasha hili ni sehemu muhimu ya kutoa mwangaza kwa watoto hawa na kuwasaidia kupitia ubunifu wa mavazi," alisema Mwanamboka.
Katika tamasha la mwaka huu, washiriki wataweza kushindania vigezo vya ubora na ubunifu wa mavazi, ambapo washindi watapatikana kutokana na kiwango cha kazi zao na mchango wao katika kuendeleza mitindo ya kisasa. Mwanamboka alisisitiza kuwa inategemewa kuwa tamasha hili litajivunia washiriki wengi kutoka maeneo mbalimbali, na litawawezesha wabunifu kutambulishwa kimataifa.

Chief Jaji wa tamasha hilo Millen Magese, alizungumza kuhusu umuhimu wa mitindo katika ulimwengu wa leo, akisema kuwa "Fashion ni zaidi ya mavazi; ni njia ya kuonyesha heshima kwa utamaduni wa nchi yetu." Aliongeza kuwa uandaaji wa vazi la Samia ni njia ya kuhakikisha urithi wa mavazi ya Kiafrika unahifadhiwa na kupitishwa kwa vizazi vijavyo. "Hii ni heshima kwa utamaduni wetu na tunapaswa kuhakikisha kuwa inakuwa sehemu ya historia yetu," alisema Magese.
Jaji Idris Sulutan pia alisisitiza umuhimu wa mitindo kama kipengele cha kuhamasisha jamii, hasa kwa wanawake. Alisema kuwa mitindo inaweza kuwa chachu kubwa ya kuwahamasisha wanawake kuwa viongozi bora katika jamii zao, na kuwawezesha kuchukua nafasi muhimu katika masuala ya kijamii na kisiasa.
"Fashion sio tu kuhusu mavazi, bali ni kuhusu kuonyesha nguvu na uwezo wa wanawake katika jamii. Tunapaswa kuwa na jukwaa hili ili kusaidia wanawake kuwa viongozi wazuri na kuchukua hatua katika uongozi wa jamii," alisema Jaji Sulutan.
Jopo la majaji litakaloshiriki katika tamasha hili linajumuisha watu maarufu katika tasnia ya mitindo, akiwemo Millen Magese, Hadija Mwanamboka, Faraja Nyarandu, Joketi Mwigelo, na Nancy Sumary. Washiriki wa tamasha hili wataweza kujivunia kuwa sehemu ya tukio hili muhimu ambalo linaendelea kuwa kivutio kikubwa katika tasnia ya mitindo nchini Tanzania na kimataifa.
Tamasha la Samia Fashion Festival linatoa jukwaa la kipekee kwa wabunifu wa mavazi na wanamitindo kuonesha vipaji vyao na kujivunia urithi wa mavazi ya Kiafrika, huku likileta hamasa kwa jamii kuhusu masuala muhimu kama afya, usawa wa kijinsia, na umoja wa kijamii.
Hakuna maoni: