ALHAJ MRUMA KUWEKA JIWE LA MSINGI MSIKITI WA MARORO MIKUYUNI.



Na Selemani Msuya,

Kilimanjaro.

KATIBU Mkuu wa Baraza la Waislam Tanzania (BAKWATA), Alhaj Nuhu Mruma kesho anatarajiwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Msikiti mpya wa Maroro Mikuyuni kata ya Mwanga wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.

Hayo yamebainishwa na Katibu wa Msikiti wa Maroro Mikuyuni, Dhahiri Mwanga wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii leo ikiwa imebakia siku moja kabla ya uzinduzi wa msikiti huo wa kisasa.

Mwanga amesema Katibu Mkuu wa BAKWATA Alhaj Mruma, ataambatana na Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro Sheikh Mlewa Shaban, Arusha Shaban Simba na viongozi wengine wa kidini mkoa na wilaya. 

"Kesho hapa kijijini kwetu Mikuyuni kuna tukio la kihistoria ambapo Katibu Mkuu wa BAKWATA, Alhaj Mruma anakuja kuweka jiwe la msingi la Msikiti mpya wa Maroro Mikuyuni, tunaomba wana Mwanga na viunga vyake wajitokeze kupokea uongozi huo wa Taifa na kutuchangia ili kuweza kukamilisha ujenzi," amesema Mwanga.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi, Yahaya Kambagha amesema msikiti huo wa kisasa ambao utakuwa na ghorofa moja ujenzi wake unatarajia kugharimu TZS milioni 700 hadi kukamilika kwake.

Kambagha amesema pia msikiti huo ukikamilika utawezesha waumini wa kiislam zaidi ya 300 kuswali kwa wakati mmoja.

"Huu msikiti wetu mpya hadi ukikamilika tunatarajia kutumia TSH milioni 700, utaweza kuchukua watu 300, utakuwa na ofisi, maktaba, chumba cha kuhifadhia na kuoshea maiti na huduma nyingine muhimu," amesema Kambagha.

Mwenyekiti huyo amewataka wananchi wa Mwanga kujitokeza na kuchangia ujenzi wa msikiti huo ambao utaweza kutumika kwa zaidi ya miaka 100 ijayo.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.