Na Emmanuel Kawau,
Dar es salaam.
Jiji la Dar es Salaam linatarajia kuanzisha mfumo wa ufanyaji biashara kwa saa 24 kwa mara ya kwanza, hatua inayolenga kuboresha uchumi na kubadilisha sura ya jiji hilo kama kitovu cha biashara nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameyasema hayo wakati akitoa taarifa ya mwisho wa mwaka ya mkoa wa Dar es salaam pamoja na salamu za Siku ya Krismas na mwaka mpaya ambapo amethibitisha hilo kuwa huduma hiyo itazinduliwa rasmi mwezi Januari 2025 katika eneo la Kariakoo, kabla ya kusambazwa katika maeneo mengine yatakayobainishwa na viongozi wa wilaya na halmashauri.
Bw. Chalamila amesema kuwa mpango huo ni sehemu ya jitihada za serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha shughuli za kiuchumi, kuongeza fursa za ajira, na kuboresha ustawi wa wakazi wa Dar es Salaam na watanzania wote kwa ujumla.
"Tunataka jiji letu lifanye kazi masaa 24, na mfumo huu utafungua milango zaidi ya uwekezaji na huduma bora kwa wananchi," alisema.
Mbali na biashara ya saa 24, Bw. Chalamila alitoa taarifa kuhusu maendeleo ya miundombinu kupitia Mradi wa Kuboresha Maeneo ya Mijini (DMDP). Ambapo amesema kuwa wakandarasi wa miradi hiyo wamekabidhiwa jukumu la kujenga barabara zenye urefu wa kilomita 255 na mifereji ya maji ya kilomita zaidi 90 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam ambapo Miradi hiyo, inayotarajiwa kuanza rasmi mwezi Januari 2025, huku ikilenga kupunguza changamoto za usafiri na kudhibiti mafuriko katika maeneo ya mijini.
Aidha, ameeleza kuwa huduma ya maji safi jijini Dar es Salaam imeanza kurejea baada ya changamoto ya kukosekana majinkwa kinpindi fulani ambapo amesema kuwa hali hiyo haikusababishwa na sababu nyingine zaidi ya uchakavu wa miundombinu. Ambapo Shirika la DAWASA linaendelea na juhudi za kuboresha huduma hiyo ili kuhakikisha wananchi wanapata maji kwa uhakika.
Akihitimisha hotuba yake kwa waandishi wa habari, Bw. Chalamila aliwatakia wakazi wa Dar es Salaam heri ya Krismasi na Mwaka Mpya. Alisisitiza umuhimu wa kusherehekea siku kuu kwa amani na kufuata sheria, huku akiwataka wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao ili kuhakikisha usalama wao.
Pia alikemea uvumi wa matukio ya utekaji ulioenea mitandaoni, akisema kuwa matukio mengi hayana ukweli na yanakusudia kuzua taharuki. Alitoa mfano wa tukio la hivi karibuni lililoripotiwa Temeke, ambapo ilidaiwa mtoto ametekwa. Baada ya uchunguzi wa kina na juhudi za jeshi la polisi, ilibainika kuwa mtoto huyo alikutwa akiwa amepoteza maisha baada ya kutumbukia kisimani katika madrasa alipokuwa akisoma, kinyume na madai ya awali ya kutekwa.
Mkuu wa Mkoa alihimiza wakazi wa jiji hilo kuwa sehemu ya jitihada za maendeleo na kudumisha amani kwa manufaa ya wote.
Hakuna maoni: