MAMA ONGEA NA MWANA NA JKCI WAANDAA KAMPENI MAALUMU YA HUDUMA AFYA BURE KWA WASANII.

Published from Blogger Prime Android App

DAR ES SALAAM.

Katika juhudi za kuimarisha ustawi wa wasanii na jamii kwa ujumla, kampeni maalum ya kupima afya ya moyo kwa wasanii imeandaliwa na Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI). Kampeni hiyo itaanza Desemba 21, 2024, na kuendelea hadi Januari 2025, ikiwa na lengo la kuwahamasisha wasanii kuchukua hatua za kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Published from Blogger Prime Android App
Steve Mengele, maarufu kama Steve Nyerere, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao, amesema kampeni hii inawalenga zaidi wasanii wa filamu, kwani wao ni miongoni mwa watu muhimu wanaohamasisha jamii. “Wasanii wanapaswa kuwa mifano bora kwa jamii kwa kuonesha kuwa afya njema ni kipaumbele. Kupima afya mara kwa mara siyo tu kunachangia maisha bora, bali pia kunawawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi,” amesema Steve.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ikiwemo magonjwa ya moyo, ni changamoto kubwa inayoweza kuepukika kwa kufahamu hali ya afya mapema na kuchukua hatua stahiki. Aliwasihi wasanii kujisajili kupitia Bodi ya Filamu Nchini na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ili kupata fursa ya huduma hizi bila gharama yoyote.

Published from Blogger Prime Android App
Dkt. Peter Kisenge, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, ameonyesha wasiwasi juu ya kuongezeka kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza nchini, ambayo yanasababisha asilimia 9 ya vifo vyote kwa mwaka. “Ni muhimu kwa wasanii, kama kioo cha jamii, kuhamasisha mabadiliko ya mtazamo kuhusu afya. Kwa kushirikiana, tunaweza kupunguza mzigo wa magonjwa haya kwa kuongeza uelewa kuhusu ulaji bora na umuhimu wa uchunguzi wa mara kwa mara,” amesema Dkt. Kisenge.

Published from Blogger Prime Android App
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa BASATA, Dkt. Kenmond Mapana, amepongeza juhudi hizi na kuahidi ushirikiano endelevu na wasanii. Amehimiza wasanii wote kujitokeza kwa wingi siku ya kampeni katika viwanja vya Kawe ili kupima afya zao.

“Hii ni fursa adhimu ya kuonesha mshikamano wetu kama sekta ya sanaa. Afya bora ni nyenzo muhimu kwa maendeleo ya kazi zetu, na tunapaswa kuweka kipaumbele katika suala hili,” amesema Dkt. Mapana.

Kampeni hii pia ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameonyesha juhudi kubwa katika kuhakikisha huduma za afya zinawafikia Watanzania wote.

Wasanii na wananchi kwa ujumla wanahimizwa kuchukua nafasi hii siyo tu kwa ajili ya afya zao binafsi, bali pia kwa lengo la kuimarisha nguvu kazi ya taifa.

Published from Blogger Prime Android App

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.