

GEITA.
Wakala wa Nishati Vijijini (REA); tarehe 10 Desemba, 2024 imeendesha mafunzo maalum kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kushirikiana na Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (TAMAVITA) na kisha kugawa majiko ya gesi ya kilo 6 kwa Watu wa makundi maalum wakiwemo Viziwi, Wasioona na wenye Ualbino wapatao 64 wilayani Bukombe, mkoani Geita.Akiongea katika hafla hiyo; Katibu Tawala wa wilaya ya Bukombe, Bwana Ally Mketo ameishukuru REA kwa kuendesha mafunzo kuhusu matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia kwa Watu wa makundi maalum wakiwemo (Wasioona, Viziwi na wenye Ualbino) katika wilaya ya Bukombe, mkoani Geita.
“Ndugu zangu kama mnavyofaham nchi yetu sasa inatoka kutoka kwenye matumizi ya nishati za “kimila”; zisizo safi na salama kama kutumia kuni, kutumia mikaa na vinyesi vya ng’ombe kwa ajili ya nishati ya kupikia na sasa tunaelekea kwenye matumizi ya nishati safi na salama, nishati ambazo hazina athari kiafya na kwa mazingira”. Amesema Katibu Tawala wa wilaya, Ally Mketo.
Ameongeza kuwa siku za nyuma Wazee katika maeneo mengi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa, walikuwa wanauwawa kwa kuhusishwa na imani za kishirikina kutoka na macho yao kuwa mekundu ambapo hali hiyo ilichangiwa na matumizi ya nishati zisizo safi na salama (Kuni na mkaa).
Bwana Mketo ametoa wito kwa Washiriki wa mafunzo hayo kuendelea kutumia nishati safi na salama ili kulinda afya zao pamoja na kulinda na kuhifadhi mazingira ambayo kwa kiasi kikubwa, yameribiwa kutokana na kukatwa hovyo kwa miti kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa.
Naye Mkufunzi, aliyeendesha mafunzo hayo kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA); Mhandisi, Kelvini Tarimo amesema lengo la mafunzo hayo kuhamasisha na kuwajengea uelewa Wananchi kwa kuwa Serikali imekusudia kuwa makundi yote ya Watu kwenye jamii wanafikiwa kwa kuwa nishati ya kupikia inatumiwa na kila mtu.
“Lengo la Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watazania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia, ili kufika huko tunaendelea kutoa elimu kwa makundi yote ya Watu ili wale wanapata mafunzo kama haya, wakaanze kutumia teknolojia za nishati safi ya kupikia na pia wakawe Mabalozi kwa wengine katika kuendeleza jitihada hizi za Serikali katika kuwaendeleza wengine katika matumizi ya nishati safi na salama.”Amesema, Mhandisi Kelvini Tarimo kutoka REA.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (TAMAVITA); Bwana Kelvin Nyema, ameishukuru REA kwa kuendesha mafunzo hayo ya nishati safi ya kupikia na kisha kugawa majiko ya gesi kwa Watu wa makundi maalum (Viziwi, Vipofu na Wenye Ualbino).
“Mafunzo haya tuliyopata ni mazuri sana kwa kuwa yametuongezea uelewa kwa sisi viziwi, vipofu na walemavu wengine walioshiriki hapa; tunamshukuru Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko kwa kuwa tulimuomba kuhusu kupata mafunzo haya, na leo REA wamekuja na kutufundisha”
Pili, tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ruzuku kwenye majiko ya gesi. Leo, Washiriki wa mafunzo haya, tumepata majiko 64”. Amesema, Bwana Nyema.
MWISHO!
*REA YAANZA KUTEKELEZA AGIZO LA SERIKALI LA KUSAMBAZA MAJIKO YA GESI WILAYANI CHATO*
*Majiko ya gesi 3,255 yaanza kununuliwa kwa bei ya ruzuku*
Wananchi wilayani Chato mkoa wa Geita wanaendelea na zoezi la kununua majiko ya gesi ya kilo 6 yapatayo 3,255; kutoka kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kupitia msambazaji, kampuni ya MANJIS Logistic Ltd ambapo tarehe 7 Disemba, 2024 katika kijiji cha Msilale Katibu Tawala wa wilaya hiyo Bwana Thomas Dimme alishiriki kwenye zoezi la ugawaji wa majiko hayo na kusisitiza kuwa ipo haya Serikali kuongeza mgao wa majiko hayo kwa kuwa mwamko ni mkubwa.
Bwana Thomas Dimme amesema Viongozi wa wilaya wanaendelea na zoezi la kuwahamasisha Wananchi ili wajitokeze kwa wingi katika kata za wilaya hiyo ili wanufaike na fursa hiyo ya kununua majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku ya shilingi 17,500 ambayo Serikali imewalipia kupitia REA badala ya shilingi 35,000, bei ya awali.
“Kwa upande wetu, tunaendelea kuwahamasisha Wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ili wajitokeze kwa wingi kununua majiko haya, yanayotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita kupitia REA kwa bei ya punguzo ya asilimia 50.” Ameeleza, Katibu Tawala wa wilaya, Bwana, Dimme.
Aidha, Dimme ameiomba Serikali kuongeza mgao zaidi katika wilaya ya Chato kwa kuwa uhitaji ni mkubwa pamoja na kuomba ruzuku kwenye gharama ya kujaza mitungi hiyo mara gesi itakapoisha.
“Sisi Wilaya yetu tupo wengi, tunazaa kwa wingi, niombe Mamlaka (Serikali) watuongezee mgao zaidi, jambo la pili tunaomba waweke utaratibu wa ruzuku ya kuweza kujaza hii mitungi.” Amesema Bwana Dimme.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Miradi kutoka REA, Mhandisi, Francis Manyama amesema ili Mwananchi apate jiko hilo la gesi, anatakiwa kuja kwenye vituo vilivyotangazwa kwa ajili ya kugawa majiko hayo akiwa na Kitambulisho cha NIDA au namba ya NIDA pamoja na shilingi 17,500.
“Serikali kupitia REA inatekeza mikakati hii, Lengo kuu ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania, wawe wanatumia nishati safi ya kupikia”. Amesema, Mhandisi, Manyama.
Itakumbukwa, tarehe 2 Disemba, mwaka huu, Mkuu wa mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigela, aliupokea rasmi Mradi kusambaza majiko hayo ya gesi yapatayo 16,275 kwa mkoa mzima; majiko yenye thamani ya shilingi milioni 285 katika hafla iliyofanyika ofisi kwake na alitoa wito kwa Wananchi kuchangamkia fursa hiyo.
MWISHO!
Hakuna maoni: