SERIKALI YAOKOA BILIONI 58.4 KUUNGWA KWA MKOA WA KIGOMA KWENYE GRIDI YA UMEME YA TAIFA.

 






Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mha. Gissima Nyamo-Hanga akiwa na viongozi wengine TANESCO hivi karibuni wametembelea Mradi wa Kituo cha Kupokea, Kupoza na Kusambaza Umeme cha Kidahwe Kigoma (400/220/132/33kV) kujionea maendeleo ya uendeshaji wa Kituo hicho baada ya kuunganishwa kwenye Gridi ya Umeme ya Taifa hivi karibuni ambapo amesema hatua hiyo imefanya Serikali kuokoa kiasi cha Shilingi Bilioni 58.4 ambazo awali zilikuwa gharama zikitumika kwa mwaka kuzalisha umeme kwa mafuta ya dizeli Mkoani humo.

Akizungumzia juu ya kuimarika kwa huduma ya umeme, Mha. Gissima amesema kuwa huduma ya umeme katika Mkoa wa Kigoma sasa itakuwa bora zaidi kwa sababu wananchi wameanza kupata umeme kutoka Gridi ya Umeme ya Taifa hatua ambayo inatoa fursa za kujitanua katika kuendesha shughuli mbalimbali zenye mahitaji ya matumizi ya umeme.

"Mbali na Mradi huu wa Kituo cha Kidahwe, tutaendelea na ujenzi wa Kituo kingine kikubwa zaidi chenye uwezo wa MVA 240 katika eneo hili la Kidahwe kwa ajili ya kuongeza wigo wa upatikanaji wa umeme ukizingatia shughuli za kiuchumi katika Mkoa huu zinakua kwa haraka, sisi kama Shirika tukaona tuongeze mradi huo ambao unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba, 2026" alieleza Mha. Gissima.

Amesema kuwa, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na TANESCO imejenga njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma kwenye Kituo cha Kidahwe yenye urefu wa kilomita 280 njia ambayo imewezesha Mkoa wa Kigoma kuungwa kwenye Gridi ya Umeme ya Taifa.

Ameongeza kuwa, matumizi ya umeme katika Mkoa wa Kigoma yanatarajiwa kupanda mpaka kufikia Megawati 22 kutoka Megawati 17.5 za sasa kwa sababu Kituo hiko cha Kidahwe kina uwezo wa Megawati 54 ambazo zinazidi mahitaji ya Mkoa huo.

Sambamba na hilo, amesema kuwa mbali na kuwepo kwa Mradi wa Kituo cha Kidahwe, upo mradi mwingine unatekelezwa kwa lengo la kuvipatia umeme vijiji 18 ambavyo vipo jirani na mradi huo wa Kidahwe na hivyo jumla ya wateja elfu tano (5000) wataunganishiwa umeme mara baada ya mradi huo kukamilika na kufanya ongezeko la wateja kutoka idadi ya wateja laki moja na elfu kumi na moja (111,000) ya sasa.

Mradi wa Kituo cha Kidahwe ni mojawapo ya miradi ya kimkakati iliyotekelezwa na TANESCO kwa lengo la kuhakikisha mikoa yote nchini inafikiwa na Gridi ya Umeme ya Taifa.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.