WAZIRI ULEGA AWAKALIA KOONI WAKANDARASI WA MIRADI YA BRT.

 



NA MWANDISHI WETU


WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amewaagiza wakandarasi wanaojenga barabara za Mradi wa Mabasi Yanayoenda Haraka (BRT) mkoani Dar es Salaam kuhakikisha ujenzi unakamilika kabla ya msimu wa mvua za masika mapema mwakani ili kupunguza changamoto za msongamano wa magari katika jiji hilo. 

Ulega ametoa maagizo hayo wakati wa ziara yake ya kushtukiza usiku wa kuamkia leo Jumamosi tarehe 28, Disemba 2024 yenye lengo la kukagua maendeleo ya miradi ya ujenzi wa miundombinu ya BRT katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam. 

"Nimeagiza kazi ifanyike usiku na mchana kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati. Msimu wa Masika una changamoto zake, na hatutaki kuona wananchi wakitaabika. Tunafanya hivi kwa kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Ilani ya CCM ya 2020-2025 inayosisitiza kupunguza msongamano wa magari mijini," amesema Waziri Ulega.

Katika ziara yake hiyo , Waziri Ulega alikagua maendeleo ya upanuzi wa barabara ya BRT 1 kutoka Ubungo hadi Kimara pamoja na barabara ya Mwenge kuelekea Tegeta inayojumuishwa katika mradi wa BRT 4. 

Amesema, ameridhishwa na kasi ya kazi zinazofanywa na wakandarasi ambao wameanza kutekeleza agizo lake la kufanya kazi saa 24 kila siku.

"Timu ya usimamizi ya Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), chini ya Mtendaji Mkuu wake, Mhandisi Mohamed Besta, inafanya kazi nzuri. Wakandarasi lazima wafanye kazi muda wote bila kupoteza muda. Watanzania wanatamani kuona miradi hii ikikamilika, na sisi kama serikali tunajali maslahi yao," ameongeza Waziri Ulega.

Kwa upande wake, Mhandisi Mohamed Besta amemhakikishia Waziri kuwa TANROADS itaendelea kusimamia wakandarasi kwa karibu ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati. 

"Tutaendelea kufanya hivi (kusimamia wakandarasi kufanya kazi usiku na mchana) Hata pale ambapo Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi hautakuja kufanya ziara za kushtukiza, tutahakikisha kazi inaendelea kwa kasi ili kufanikisha lengo la kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam," amesema Mhandisi Besta.

Naye Meneja wa Mradi wa BRT, Mhandisi Allen Natai, ameeleza kuwa kazi ya kujenga miundombinu ya barabara za mabasi yaendayo haraka inaendelea vizuri. 

Ziara ya Waziri Ulega imeoneesha dhamira ya serikali ya kuhakikisha miradi mikubwa ya maendeleo inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa ili kuboresha huduma kwa wananchi na pia imetoa msukumo mpya kwa utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) jijini Dar es Salaam.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.