MBEYA.
Makusanyo ya maduhuli ya Serikali kupitia sekta ya madini katika Mkoa wa Mbeya, yatokanayo na mrabaha, tozo na ada mbalimbali, kwa mwaka wa fedha ulioanza Julai 2024/2025, yamefikia jumla ya Shilingi bilioni 2.3. Kiasi hiki ni sawa na asilimia 63 ya lengo la mwaka na asilimia 108 ya lengo la kipindi cha miezi saba (Julai 2024 hadi Januari 2025).
Akizungumza kwa niaba ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Migodi William Kajumla amesema kuwa Mkoa wa Mbeya ulipangiwa kukusanya Shilingi bilioni 3.7.
Ameeleza kuwa mapato makubwa katika Mkoa wa Mbeya yanatokana na madini ya viwandani, dhahabu na madini ujenzi, pamoja na miradi mbalimbali ya barabara.
“Tunategemea mapato kutoka kwenye kiwanda kinachozalisha hewa ya ukaa cha TOL Gas Rungwe, na Kiwanda cha Saruji ‘Mbeya Cement’ kwa madini ya viwandani, lakini pia biashara ya dhahabu na machimbo madogo madogo ya madini ujenzi,” amesisitiza.
Aidha, Mhandisi Kajumla ametoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika Mkoa wa Mbeya, hususan sekta ya madini ujenzi, makaa ya mawe Ngana Kyela na Rungwe, pamoja na uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu kwenye maeneo ya Mabadaga, Msesule na Madibira wilayani Mbarali, pamoja na Lwanjiro, Ileya, Ishinda na Chikula wilayani Mbeya.
Hakuna maoni: