DAR ES SALAAM, JUNI 23,2025
Jiji la Dar es Salaam limekuwa mwenyeji wa mkutano muhimu unaowakutanisha wawakilishi kutoka mataifa 15 ya Afrika, wakijadili kwa kina maboresho ya mikataba ya nyuklia, kwa lengo la kuwezesha utekelezaji salama wa miradi ya nyuklia inayolenga ustawi wa kijamii na ukuaji wa uchumi.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, alibainisha kuwa Tanzania kwa kushirikiana na Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Nyuklia (IAEA), imeandaa kikao hicho ili kuhakikisha vyanzo vya nyuklia vinatumika kwa njia salama bila kuathiri binadamu wala mazingira.
"Ni hatua muhimu kwa mataifa wanachama kuhakikisha kuwa utekelezaji wa miradi ya nyuklia unaendana na viwango vya kimataifa vya usalama na uendelevu," alisema Prof. Mushi. Alisisitiza kuwa matumizi ya teknolojia ya nyuklia lazima yalete faida halisi kwa jamii na kuchochea maendeleo ya nchi husika.
Kwa upande wake, Prof. Najat Kassim Mohamed, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomic Tanzania (TAEC), alieleza kuwa mikakati mbalimbali ya kimataifa imeandaliwa ili kuhakikisha matumizi bora na salama ya nyuklia, ambapo utekelezaji wake unaweza kuchukua kati ya miaka saba hadi kumi.
"Tanzania ina nafasi muhimu kutokana na kuwa na vyanzo kadhaa vya nyuklia vyenye uwezo wa kuchangia maendeleo, na pia kuwa njia ya kupitisha vifaa au malighafi za nyuklia kwa mataifa jirani yasiyo na bandari," alisema Prof. Najat.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TAEC, Bw. John Simba Chaka, aliongeza kuwa mkutano huo pia unatoa fursa kwa nchi shiriki kubadilishana uzoefu kuhusu namna bora ya kushughulikia usafirishaji wa madini ya nyuklia, ambayo yanatumika katika sekta mbalimbali duniani.
Kupitia mkutano huu, Afrika inaonesha mshikamano wake katika kulinda rasilimali nyuklia na kuhakikisha matumizi yake yanasaidia kuinua maendeleo ya kisayansi, kijamii na kiuchumi kwa mataifa ya bara hili.
Hakuna maoni: