BARAZA LA MADIWANI JIJI LA DAR ES SALAAM LAVUNJWA RASMI; DC MPOGOLO ATOA UHAKIKA WA UKAMILISHAJI WA MIRADI YA MAENDELEO
Dar es salaam, Juni 20,2025.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Edward Mpogolo, amewahakikishia wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuwa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji hilo itakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

DC Mpogolo alieleza kuwa mafanikio haya yanatokana na ushirikiano madhubuti baina ya watendaji wa Halmashauri wakiongozwa na Mkurugenzi Mabelya, ambao amewasifu kwa kuwa na maono, ufanisi na uwajibikaji mkubwa.
“Kwa kweli tuna timu imara. Mkurugenzi Mabelya pamoja na wataalamu wake wanafanya kazi kwa moyo mmoja, na hiyo imetufikisha hapa tulipo leo. Tuna uhakika kuwa miradi yote iliyopangwa itakamilika kwa ubora unaopaswa,” alisema DC Mpogolo.
Aidha, alitumia nafasi hiyo kutoa pongezi kwa Mstahiki Meya Omary Kumbilamoto na Baraza zima la Madiwani kwa kazi nzuri ya kusimamia ukusanyaji wa mapato pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayowanufaisha wananchi moja kwa moja.
Kuvunjwa kwa Baraza hilo ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, aliyetaka mabaraza yote ya madiwani nchini kuvunjwa kufikia Juni 20, 2025 kutokana na kumalizika kwa muda wa uongozi wa Serikali za Mitaa kwa mujibu wa sheria.
Hakuna maoni: