KIKWETE AWATAHADHARISHA WATANZANIA: CHAGUENI VIONGOZI KWA HOJA, SI KELELE – ASEMA KWENYE KONGAMANO LA SHERIA KUELEKEA UCHAGUZI 2025
Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete amewataka Watanzania kuwa makini kwa kuchambua kwa kina hoja za wanasiasa ili kupata viongozi bora wa kuliongoza taifa.
Kikwete alitoa kauli hiyo katika Kongamano la Kitaifa la Sheria kuelekea Uchaguzi Mkuu, akibainisha kuwa mabadiliko ya sheria yamekuwa yakifanyika katika vipindi tofauti tangu awamu ya nne hadi awamu ya sita ya uongozi, ikiwa ni jitihada za kuhakikisha ushiriki mpana wa wananchi katika uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani.
"Kwa mfano, mwaka 2024 kulifanyika maboresho ya masharti yanayohusu wasimamizi wa uchaguzi na wakurugenzi. Kwa sasa ni Tume Huru ya Uchaguzi inayowateua wasimamizi, jambo linaloimarisha uwazi na uhuru wa uchaguzi,” alisema Dkt. Kikwete, huku akionya dhidi ya upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu kuhusu mabadiliko hayo.
Aliongeza kuwa moja ya maeneo yaliyofanyiwa marekebisho ni kuondoa utaratibu wa mgombea kupita bila kupingwa, hatua ambayo alisema ni muhimu katika kuimarisha demokrasia nchini.
Aidha, alieleza kuwa sheria nyingi sasa zimeandikwa kwa Kiswahili ili kuwawezesha wananchi wengi kuzielewa kwa urahisi, jambo linalosaidia kuongeza ushiriki wa wananchi katika masuala ya kisheria na kisiasa.
“Pamoja na hatua hizi, bado hatujafika mwisho. Tunapaswa kufanya vizuri zaidi ili kila Mtanzania atimize haki yake ya msingi ya kuchagua na kuchaguliwa,” alisisitiza Kikwete.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TLS), Bavoo Junus, alisema lengo la kongamano hilo ni kuwapa wananchi elimu muhimu kuhusu sheria za uchaguzi.
Alibainisha kuwa elimu hiyo ni muhimu kwa kuwawezesha Watanzania kushiriki kwa haki, amani na uelewa katika mchakato mzima wa kidemokrasia kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.
Hakuna maoni: