Dar es salaam, Juni 18,2025.
Salum Ismaili Salum, ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa UVCCM kwa Vyuo na Vyuo Vikuu Mkoa wa Dodoma, ametangaza nia yake ya kugombea Ubunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Mkoa wa Shinyanga, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Salum amesema kuwa maono ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwaamini na kuwawezesha vijana yamechochea hamasa yake ya kujitosa kwenye siasa za ubunge.
Salum amesema kuwa dhamira yake ni kushirikiana na wananchi kuharakisha maendeleo ya Kahama, kwa kutumia fursa mbalimbali zilizopo ikiwemo uwepo wa rasilimali madini, ardhi yenye rutuba, na idadi kubwa ya vijana ambao wanaweza kuhamasishwa katika uzalishaji na ujasiriamali.
“Jimbo la Kahama lina nafasi kubwa ya kuimarika kiuchumi ikiwa tutatumia vizuri rasilimali tulizonazo. Nataka kuwa sauti ya mabadiliko chanya kwa wananchi,” amesema.
Amesema anatarajia kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo tarehe 28 Juni, 2025, mara tu dirisha la uteuzi litakapofunguliwa.
Katika hatua nyingine, Salum amewaonya baadhi ya wanasiasa na wanaharakati wanaotumia jukwaa la siasa kuchochea hofu na machafuko. Ametoa wito kwa Watanzania kuendeleza mshikamano, huku akisisitiza kuwa vijana wa CCM hawatakubali kuona nchi ikiingizwa kwenye vurugu za kisiasa.
Akiwapongeza viongozi waliotangulia, Salum amesema kuwa tangu kuingia madarakani kwa Rais Samia, miradi mingi ya kimkakati imeboreshwa na mingine kukamilishwa, hatua ambayo imeongeza imani kwa wananchi.
Ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais kwa kazi nzuri anayoifanya, akieleza kuwa mafanikio ya sasa ni matokeo ya uongozi imara na maono ya mbali.
“Hatutasita kukemea wanaomdhalilisha Rais wetu. Tunahitaji siasa safi na yenye heshima kwa ustawi wa taifa,” amesema.
Hakuna maoni: