MAKAMU WA RAIS DKT. MPANGO AONDOKA NCHINI KWENDA UFARANSA KUMWAKILISHA RAIS SAMIA KWENYE MKUTANO WA KIMATAIFA KUHUSU BAHARI
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, ameondoka nchini leo tarehe 7 Juni 2025 kuelekea Jijini Nice, Ufaransa, kwa ajili ya kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Bahari (UNOC3).
Mkutano huo wa kimataifa unatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 9 hadi 13 Juni 2025 na unalenga kuhamasisha utekelezaji wa Lengo la Maendeleo Endelevu namba 14 (SDG 14), linalojikita katika kuhifadhi na kutumia kwa uendelevu rasilimali za bahari, bahari kuu, na mazingira ya pwani.
UNOC3 ni jukwaa muhimu linalowakutanisha Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, mashirika ya kimataifa, asasi za kiraia pamoja na sekta binafsi ili kujadili masuala ya bahari na namna bora ya kuzitumia kwa maendeleo endelevu.
Katika ziara hiyo, Makamu wa Rais anatarajiwa kushiriki katika mikutano mbalimbali ya uwili (bilateral meetings) inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na mashirika pamoja na mataifa mbalimbali yanayoshiriki mkutano huo.
Kupitia ushiriki huo, Tanzania inatarajia kuimarisha nafasi yake katika jamii ya kimataifa, kujenga ushirikiano mpya na kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali kwa ajili ya maendeleo ya uchumi wa buluu nchini.
Hakuna maoni: