Na Ahmada John,
Zanzibar.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kuwa chama cha ACT Wazalendo hakiwezi kuafikiana na ukweli wowote kati yake na CCM, kwani kila wakati hufikiri kwamba demokrasia ya kweli ni CCM kuondoka madarakani.
Pia, CCM kimekanusha kuwepo kwa waraka wowote au makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande hizo mawili kuhusu kugawana madaraka.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, ambaye alisema kitendo cha Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman (OMO), kuwalalamikia wanadiaspora akiwa Uingereza ni matumizi mabaya ya muda.
Mbeto alieleza kuwa makubaliano ya msingi kati ya CCM na ACT Wazalendo ni kuendeleza Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
“Si kweli kama kulikuwa na mpango wa kugawana madaraka kama inavyodaiwa na Othman, hata wakati wa Hayati Maalim Seif Sharif Hamad alipokuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa SMZ,” alisema.
Aidha, alisisitiza kuwa hakuna kipengele chochote katika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kinachotaja kugawana madaraka ndani ya SMZ.
Mbeto aliongeza kuwa hata walipokutana aliyekuwa Rais wa Zanzibar wa Awamu ya Saba, Dk Amani Karume, na Hayati Maalim Seif, hakukuwa na kabrasha la makubaliano yoyote yaliyoandikwa kuhusu kugawana madaraka.
“Makubaliano ya msingi yalifikiwa baada ya Baraza la Wawakilishi kufuta kipengele cha katiba kilichotaka anayeshinda achukue vyote, na kutangaza kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar,” alieleza.
Mbeto alisema kuwa mjadala kuhusu kugawana madaraka haukuwahi kufikia tamati, tangu mazungumzo ya kutafuta suluhu yaliyofanyika Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, ambapo wajumbe wa CUF walisusia mazungumzo hayo.
“Mazungumzo yaliyogusia kugawana madaraka yalifanyika kati ya CCM na CUF, siyo ACT Wazalendo. Hata hivyo, mazungumzo hayo yalivunjika baada ya viongozi wa CUF kuikimbia meza ya majadiliano,” alisema.
Alibainisha kuwa baada ya viongozi wa CUF kujiondoa kwenye mazungumzo hayo, Dk Karume na Maalim Seif walikutana faragha Ikulu tarehe 9 Novemba 2009 na kufikia muafaka usio rasmi wala wa maandishi.
“OMO hajui yaliyojadiliwa kwa kuwa wakati huo hakuwa mwanachama wa CUF wala wa ACT. Anasimuliwa tu na kupotoshwa na wanaompa taarifa hizo. Aonyeshe kabrasha la makubaliano kati yake na Rais Dk Mwinyi au na Maalim Seif,” alisisitiza Mbeto.
Hakuna maoni: