MCHUNGAJI HANANJA: MAKANISA YANAYOKIUKA SHERIA YAFUNGIWE KULINDA AMANI YA TAIFA


Dar es Salaam, Juni 09,2025.

Mchungaji mstaafu kwa hiari wa kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania (KKKT),na Mkurugenzi wa Taasisi ya Hananja Compassion Foundation, inayojihusisha na kuwahudumia watu wanaotumia dawa za kulevya, Richard Hananja, ametoa wito kwa Serikali kuyafungia makanisa yote yanayokiuka sheria na taratibu za usajili, ili kudumisha amani ya taifa.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mchungaji Hananja alisema kuwa kuna ongezeko la makanisa ambayo hayafuati taratibu rasmi, jambo linalosababisha taharuki ndani ya jamii.


"Hapingi maoni ya watu," alisema, "lakini kuna viongozi wa dini wanaotumia vibaya madhabahu kwa kuwatukana viongozi wa serikali, kutoa kashfa na kuzusha mivutano."


Akizungumzia kuhusu baadhi ya matamko yanayohusiana na masuala ya utekaji, alisema:

"Kwani haya mambo ya utekaji yameanza leo? Kwa nini wajitokeze sasa? Jiepusheni kuingilia masuala ya maslahi ya watu. Wameona uchaguzi unakaribia, sasa wanajitokeza kwa nia ya kutuvuruga."


Mchungaji Hananja alisisitiza kuwa viongozi wa dini wana nafasi ya kuwasiliana na viongozi wa juu wa serikali kama Rais kupitia njia rasmi, badala ya kutumia madhabahu kwa matusi au kejeli.


“Ni vyema watu wakakosoa kwa uvumilivu,” aliongeza. “Kama kuna jambo haliko sawa, tuseme kwa ustaarabu, si kwa kutumia lugha chafu. Hakuna nchi duniani iliyo tulivu kabisa, lakini tusivuruge yetu kwa makusudi.”


Aliwaonya viongozi wa dini wanaoshabikia machafuko kuwa hakuna atakayenusurika iwapo nchi itaingia katika vurugu:

"Tuilinde amani yetu kwa gharama yoyote ile," alisisitiza.


Sambamba na hayo, aliwataka Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao kwa kuchagua viongozi sahihi na kujiepusha na kusambaza taarifa za uongo ambazo huweza kuleta taharuki katika jamii.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.