MSAANI D VOICE WA WCB ATANGAZA ZIARA KANDA YA ZIWA, MASHABIKI WATAKOPA SIMU KUPITIA MANDASI STORE





DAR ES SALAAM.

Msanii nguli wa muziki wa singeli nchini Tanzania, D Voice, ambaye yupo chini ya lebo ya muziki wa kizazi kipya ya Wasafi Classic Baby (WCB), ametangaza rasmi ziara maalum ya burudani katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, ikiwa ni sehemu ya kuwasogezea mashabiki wake burudani pamoja na fursa za kiuchumi. Ziara hiyo inatarajiwa kuanza rasmi katika mkoa wa Shinyanga, kabla ya kuendelea kwenye mikoa mingine ya Kanda hiyo.


Akizungumza wakati wa kutangaza ziara hiyo jijini Dar es Salaam, D Voice amesema lengo ni kuwashukuru mashabiki waliomuwezesha kufika alipo, lakini pia kuwapa nafasi ya kumwona na kufurahia burudani ya moja kwa moja. “Mashabiki wangu wamekuwa nguzo kubwa ya mafanikio yangu. Safari hii si ya muziki tu, bali ni safari ya kuwatia moyo na kuwainua kiuchumi kwa kushirikiana na wadau wetu kama Mandasi Store,” alisema D Voice.


Msanii maarufu Baba Levo ambaye ni rafiki wa karibu wa D Voice na pia mshiriki katika baadhi ya matukio ya ziara hiyo, amesema huu ni mwanzo mpya wa ushirikiano baina ya wasanii na sekta binafsi kwa ajili ya kuinua vipato vya wananchi kupitia ubunifu. “Tumeamua kutumia jina letu kwa faida ya jamii. Burudani haitakuwa mwisho, kutakuwa na elimu ya kifedha na watu wengi watapata simu kwa mkopo nafuu kabisa, jambo ambalo halijawahi kufanyika katika matamasha ya burudani ya muziki wa singeli,” alisema Baba Levo.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mandasi Store, Hamis Mandasi, amesema kampuni yao imeamua kushirikiana na WCB na wasanii kama D Voice ili kusaidia Watanzania kufikia ndoto zao kwa kuwawezesha kupata simu janja kwa urahisi. “Tunajua umuhimu wa simu katika dunia ya sasa – kwa biashara, mawasiliano na hata kujifunza. Ndio maana tumekuja na mpango wa watu kukopa simu kwa masharti nafuu. Tunaanza Shinyanga lakini lengo ni kufikia mikoa yote ya Kanda ya Ziwa,” alisisitiza Bi. Fatma.


Ziara hiyo inatarajiwa kuwa ya aina yake, ikihusisha burudani ya moja kwa moja kutoka kwa D Voice na wasanii wengine wa WCB, maonyesho ya bidhaa mbalimbali, huduma za kijamii kama vile ushauri wa kibiashara, pamoja na zoezi la usajili na ukopaji wa simu. Tayari maandalizi yamekamilika, huku mashabiki wengi wakiwa na shauku kubwa ya tukio hilo.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.