BODI YA TMA YATEMBELEA RADA YA HALI YA HEWA BANGULO, PUGU NA KITUO CHA HALI YA HEWA JNIA


Dar es Salaam, 23 Julai 2025

Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imefanya ziara ya kikazi kukagua utendaji kazi wa Mamlaka hiyo katika Kituo cha Rada ya Hali ya Hewa Bangulo, Pugu, pamoja na Ofisi za TMA zilizopo katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.

Ziara hiyo iliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Mheshimiwa Jaji Mshibe Ali Bakari, akishirikiana na Makamu Mwenyekiti wa Bodi, Dkt. Emmanuel Mpeta.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Jaji Mshibe alisema kuwa lengo kuu la ziara hiyo ni kufuatilia na kutathmini usimamizi na utendaji wa miundombinu ya TMA, utekelezaji wa maagizo ya Bodi, pamoja na kujionea maendeleo na changamoto zilizopo.“Bodi imekuwa ikitoa maelekezo mbalimbali, hivyo leo ilikuwa ni siku maalum ya kufuatilia utekelezaji wake,” alisema Jaji Mshibe.

Ameeleza kuwa TMA imepiga hatua kubwa katika kuboresha miundombinu ya utoaji wa huduma, na akaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuiwezesha Mamlaka kwa kuipatia vifaa vya kisasa.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Mabadiliko ya Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a, aliishukuru Bodi kwa kutembelea vituo hivyo na kujionea utendaji kazi wa Mamlaka, hasa katika maeneo ya uangazi, uchakataji wa data na utoaji wa utabiri wa hali ya hewa.

Dkt. Chang’a alibainisha kuwa uwekezaji katika rada za hali ya hewa umewezesha TMA kuboresha utabiri na kutoa mafunzo ya kitaalamu kwa wataalamu kutoka nchi 10 za Afrika Mashariki na Kati, jambo lililoipa Tanzania heshima kubwa katika ukanda huo.

“Serikali pia imeendelea kuhakikisha usimamizi endelevu wa mitambo hii ya kisasa kwa kuajiri na kuwajengea uwezo wataalamu husika. Mpaka sasa TMA ina wahandisi 30 waliobobea,” alieleza Dkt. Chang’a

Katika hatua nyingine, wajumbe wa Bodi walitembelea Kompyuta Kubwa ya Kisasa (Computer Cluster) yenye uwezo mkubwa wa kuchambua na kuchakata taarifa za hali ya hewa, hatua inayosaidia kuimarisha utoaji wa utabiri kwa usahihi na kwa wakati katika maeneo mbalimbali nchini.


---

#tma #haliyahewa #radasabahayahewa #mabadilikoyatabianchi #raisamiasuluhuhassan #teknolojiyakisasa #afrikamashariki #utabiriyenyeusahihi 

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.