Na Mwandishi Wetu,
Dar es salaam.
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata jumla ya kilo 37,197.142 za dawa za kulevya katika kipindi cha Mei hadi Julai mwaka huu, kufuatia operesheni mbalimbali zilizofanywa kwa kushirikiana na vyombo vya dola nchini.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam, akifafanua kuwa miongoni mwa dawa hizo, ni kilo 11,031.42 za Mitragyna Speciosa (aina mpya ya dawa za kulevya zinazotokana na mmea wa Kratom).
Aidha, dawa nyingine zilizokamatwa ni pamoja na:
🔸 Bangi: kilo 24,873.56
🔸 Mirungi: kilo 1,274.47
🔸 Skanka: kilo 13.42
🔸 Heroin: kilo 2.21
🔸 Methamphetamine: gramu 1.42
🔸 Ketamine: kilo 1.92
🔸 Flunitrazepam (Rohypnol): vidonge 1,000
🔸 Hydrochloric Acid: lita 6
🔸 Mashamba ya bangi yaliyoteketezwa: ekari 1,045.5
Kamishna Lyimo aliongeza kuwa kilo 26 za heroin zilizokuwa zikisafirishwa kutoka Msumbiji zilizuiawa kabla ya kuingia nchini, huku jumla ya watuhumiwa 64 wakikamatwa kuhusiana na biashara hiyo.
Katika operesheni ya Bandari Kavu Temeke, dawa za Mitragyna Speciosa zilipatikana zikiwa zimehifadhiwa kwenye maboksi yaliyoandikwa kuwa ni mbolea. Alieleza kuwa dawa hiyo ina kemikali aina ya Mitragynine na 7-Hydroxymitragynine (7-HMG) zinazoweza kusababisha uraibu mkubwa na hata vifo vya ghafla.
Katika tukio jingine Posta, watuhumiwa sita wakiwemo raia wawili wa China – Chein Bai na Qixian Xin, walikamatwa na dawa aina ya methamphetamine, ketamine na rohypnol. Vilevile, eneo la Sinza, watu wawili walikamatwa wakiwa na kiwanda bubu cha kutengeneza biskuti zilizochanganywa na bangi, ambazo walikuwa wakisambaza kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Lindi na Mtwara.
Mkoani Lindi, mfanyabiashara wa madini alikamatwa kwa kusambaza biskuti hizo haramu.
Kamishna Lyimo pia alieleza kuwa baadhi ya wahalifu wameanza tena kutumia maiti kama njia ya kusafirisha dawa za kulevya (maarufu kama begi), huku wakitumia mahusiano ya kirafiki kuwatumia Watanzania kama wasafirishaji kwa kutumia magari, bodaboda, bajaji, taxi na kampuni za usafirishaji mizigo.
Aliwataka wananchi kuwa makini wanapotumwa au kupokea mizigo, hasa kutoka kwa watu wasiowafahamu vyema.
"Ni muhimu mjiridhishe na mizigo mnayoisafirisha ili kuepuka kuingia kwenye mikono ya sheria. DCEA inawaomba Watanzania kuendelea kushirikiana na mamlaka kwa kutoa taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya," alisema Lyimo.
Alisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayejihusisha na uzalishaji, usambazaji au biashara ya dawa hizo haramu.
Hakuna maoni: