IVO MAPUNDA KOCHA MKUU MPYA WA TEMBO WARRIORS


Na Mwandishi Wetu,

Shirikisho la Mpira wa Miguu kwa Watu Wenye Ulemavu (TAFF) limemtangaza rasmi Ivo Mapunda kuwa Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya watu wenye ulemavu, Tembo Warriors.

Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Ufundi wa TAFF, Shaban Msangi, ambaye amesema Mapunda atahudumu katika nafasi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja, huku mafanikio yake yakifuatiliwa kwa karibu ili kuamua hatma yake ya baadaye.

Kwa mujibu wa Msangi, kutokana na maandalizi ya michuano ya Afrika Mashariki na Kati (CECAAF) inayotarajiwa kufanyika Septemba mwaka huu huko Bujumbura, Burundi, Jumatatu ijayo Mapunda atakutana na viongozi wa TAFF kupanga tarehe rasmi ya kutangaza kikosi cha timu ya taifa.

Ivo Mapunda ni mchezaji wa zamani wa timu za Simba, Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars. Mnamo mwaka 2022, aliwahi kuwa sehemu ya benchi la ufundi la Tembo Warriors kama kocha wa makipa katika michuano ya Kombe la Dunia yaliyofanyika nchini Uturuki.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.