JUSSA PILIPILI ASOILA INAMUWASHIA NINI?


Na Mwandishi Wetu, 

Zanzibar.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemshukia Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu, kikimtaka ajiandae kisaikolojia kwa kile kilichotajwa kuwa chama chake hakiwezi kustahimili mikikimikiki ya CCM ifikapo Oktoba mwaka huu.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, amesema Jussa aache ngebe na mshawasha wa kisiasa, huku akiuliza kwa kejeli: "Pilipili iko shamba, Jussa anawashwaje mitaani?"

Mbeto amesema kuwa Jussa na ACT Wazalendo wanapaswa kutambua kuwa zama za porojo na uzushi zimepitwa na wakati, na sasa ni muda wa kushuhudia maamuzi ya haki kupitia nguvu ya umma.

Aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) chini ya Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi imefanya kazi kubwa kupitia sera na mikakati madhubuti, jambo linalowafanya wananchi kuwa tayari kumrejesha madarakani kwa kishindo.

"Kila mcheza kwao hutunzwa. Kwa maendeleo yaliyopatikana, wananchi wameapa kumrudisha Dk Mwinyi madarakani. Jussa omba uhai ushuhudie kimbunga Hidaya," alisema Mbeto.

Aidha, Mbeto amesema ushindi wa CCM hautahitaji ‘tochi’ kwa sababu kazi zilizofanywa na serikali ni dhahiri mbele ya macho ya wananchi. Amedai kuwa Zanzibar chini ya Dk Mwinyi inaelekea kuwa kama Dubai, Thailand au Hong Kong ya Afrika Mashariki.

Kuhusu tuhuma kuwa Rais Dk Mwinyi anapandikiza wagombea majimboni, Mbeto amesema madai hayo ni porojo za kitoto kutoka kwa Jussa, na kwamba wagombea wote wa CCM wanajitokeza kwa utashi wao binafsi, si kwa maagizo ya viongozi.

Mbeto pia amesisitiza kuwa Rais Dk Mwinyi alikataa siasa za majibizano tangu mwanzo wa utawala wake na amekuwa akijikita kwenye kazi ya maendeleo.

"Jussa aendelee kuwapa matumaini hewa wafuasi wake, lakini ukweli utajulikana wakati wananchi watakapotoa maamuzi ya kidemokrasia," alihitimisha.


Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.