DAR ES SALAAM.
Aliyekuwa mtia nia wa nafasi ya Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndg. Masoud Hassan Maftaa, ametoa tamko la heshima na mshikamano baada ya jina lake kutokuwemo kwenye orodha ya watia nia waliopitishwa kuendelea na mchakato ndani ya chama katika Jimbo la Kinondoni, Wilaya ya Kinondo.
Akizungumza mara baada ya matokeo hayo ya mchujo kutolewa jana na Katibu wa itikadi, uenezi na mafunzo wa CCM Comrade Amosi Makala. Masoud alisema:
"Sote tunafahamu kuwa Chama Cha Mapinduzi kina kanuni zake, sheria zake, mila na desturi zake. Tulijaza fomu, zikafanyiwa mchakato na viongozi wetu kupitia majina yote. Isivyo bahati, sikuwemo kwenye majina yaliyopitishwa. Hili ni jambo la kawaida katika siasa na mashindano yoyote, ambapo mshindi mmoja hupatikana kati ya wengi."
Amepongeza uongozi wa chama kwa kazi kubwa ya kusimamia mchakato mzima na kueleza kuwa ataendelea kuwa mtiifu kwa CCM. Aidha, amesisitiza kuwa yuko tayari kushirikiana kwa ukaribu na mgombea atakayepitishwa kupeperusha bendera ya CCM katika jimbo hilo.
"Nitakuwa tayari kushirikiana naye bega kwa bega, kupita kila kona ya Jimbo la Kinondoni, kuwashawishi wanachama wetu na hata wasiowanachama kumpigia kura mgombea wa CCM ili kuhakikisha tunapata ushindi wa kishindo," amesema Masoud.
Tamko hilo la Masoud linaonesha mfano wa utii kwa chama na mshikamano wa kweli unaojengwa ndani ya CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Hakuna maoni: