MCHAKATO WA MCHUJO CCM WACHUKUA MUDA KUTOKANA NA UKUBWA WA CHAMA – MBETO

 


ZANZIBAR.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis amesema mchakato wa mchujo wa wagombea wa Ubunge, Uwakilishi na Udiwani ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) unachukua muda mrefu kutokana na ukubwa wa chama hicho na idadi kubwa ya wanachama waliojitokeza kuchukua fomu.


Akizungumza na wanahabari visiwani Zanzibar jana, Mbeto alisema kuwa mchakato huo unahusisha vikao vingi vya kupitia na kuchambua majina ya watia nia, hivyo ni jambo la kawaida kuchukua muda mrefu kabla ya kutangazwa kwa wagombea waliopitishwa.


“Vikao havijafika mwisho. Jana tarehe 10 Julai tumemaliza vikao vya ngazi ya mkoa, na leo tarehe 11 Julai ni zamu ya Sekretarieti ya Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa kufanya kazi yake,” alisema Mbeto.


Aliongeza kuwa anashangazwa na baadhi ya viongozi wa ACT Wazalendo wanaohoji kwa nini CCM haijatangaza wagombea wake hadi sasa, huku akieleza kuwa hali ya chama hicho ni tofauti kabisa kutokana na ukubwa wake.


“CCM ni chama kikubwa. Ndiyo maana unaona idadi kubwa ya wanachama wamejitokeza kuchukua fomu. Makada zaidi ya 2,098 wameomba ridhaa ya chama kwa nafasi za Uwakilishi, Ubunge na Udiwani Zanzibar, wakati kwa ACT hawazidi 300. Watajifananisha vipi na sisi?” alihoji Mbeto.


Alisisitiza kuwa hakuna hata jimbo moja ambalo ACT Wazalendo wamevuka idadi hiyo ya waombaji, hivyo kulinganisha mwenendo wa CCM na ACT ni kupoteza muktadha halisi wa mambo.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.