MWALIMU AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MAISHA KWA KULAWITI MWANAFUNZI

 



Na Mwandishi Wetu


Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita imemhukumu kifungo cha maisha mwalimu wa Shule ya Msingi Waja Springs, Josephat Masenema, baada ya kupatikana na hatia ya kumuingilia kinyume cha maumbile mwanafunzi wa darasa la tatu mwenye umri wa miaka saba.


Kwa mujibu wa hukumu iliyosomwa na Hakimu Mkazi C. Waane tarehe 3 na 18 Juni 2025, kitendo hicho ni kosa kisheria chini ya Kifungu cha 154(1)(a) na (2) cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16.


Masenema alishtakiwa kwa kesi ya jinai Na. 32126/2024, akidaiwa kutenda kosa hilo mnamo Septemba 27, 2024 katika choo cha shule hiyo iliyoko Mtaa wa Bombambili, mkoani Geita.


Upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi kadhaa, akiwemo mtoto mwenyewe, mama wa mtoto, afisa ustawi wa jamii, daktari kutoka hospitali ya serikali na maafisa wa polisi. Mahakama iliridhika kuwa ushahidi uliotolewa, hususan maelezo ya mtoto na fomu ya matibabu (PF3) iliyothibitisha kuwepo kwa majeraha, ulithibitisha kosa hilo pasina shaka.


Licha ya mshitakiwa kujitetea kwamba siku ya tukio ilikuwa siku ya michezo na kwamba alikuwa na walimu na wanafunzi wengine uwanjani, mahakama ilitupilia mbali utetezi huo kwa kushindwa kuthibitishwa.


Hakimu Waane alihitimisha kuwa ushahidi uliowasilishwa umethibitisha bila shaka kwamba Masenema alitenda kosa hilo na kwa kuwa mtoto ana umri wa miaka nane sasa, adhabu sahihi ni kifungo cha maisha gerezani.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.