UZINDUZI WA DIRA YA MAENDELEO 2050 KUFANYIKA JULAI 17 DODOMA ,RAIS SAMIA KUONGOZA SHUGHULI HIYO


JULAI 08,2025, DAR ES SALAAM.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza hafla rasmi ya uzinduzi wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 itakayofanyika Julai 17, 2025 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.


Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, alipokuwa akizungumza na wanahabari kupitia Jukwaa la Wahariri (TEF), jijini Dar es Salaam. Uzinduzi huo utaambatana na Mkutano wa Tatu wa Kitaifa kuhusu Dira ya Maendeleo.


Prof. Mkumbo amesema kuwa maandalizi ya Dira 2050 yalifanyika kwa kushirikisha wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi, ambapo mchango wa wananchi kutoka makundi tofauti ulichangia kwa kiasi kikubwa katika kuunda msingi wa dira hiyo.


“Dira hii haibebi maslahi ya chama chochote cha siasa, bali ni mwongozo wa taifa zima. Vyama vinapaswa kuiakisi dira hii kwenye sera na ilani zao,” alieleza Prof. Mkumbo.


Aliongeza kuwa maoni ya Watanzania yalitolewa kupitia mikutano ya ushirikishwaji wa wadau, ikiwemo vyombo vya habari, mashirika ya kiraia, sekta binafsi, vyama vya siasa, wasomi pamoja na makundi ya kijamii.


Katika hatua ya kuandaa dira hiyo, serikali ilituma timu ya wataalamu kujifunza kutoka nchi kadhaa zilizofanikiwa kupiga hatua kubwa za kimaendeleo kama Morocco, Mauritius, Kenya, Afrika Kusini, China, India, Indonesia, Singapore, Vietnam na Korea Kusini.


“Vietnam na Singapore walitufundisha umuhimu wa kuongeza thamani ya bidhaa na kuwekeza kwenye dira madhubuti ya maendeleo. Ni somo kubwa kwetu kama taifa,” alisema Prof. Mkumbo.


Baada ya hatua ya ukusanyaji wa taarifa, rasimu ya kwanza ya dira iliwasilishwa kwa wananchi kupokea maoni. Baadaye, rasimu hiyo ilifanyiwa marekebisho na kuwasilishwa kwa Waziri Mkuu, kisha kwa Waziri wa Mipango na Uwekezaji ambaye aliiongoza hadi hatua ya kupitishwa na serikali.


Mnamo Juni 22, 2025, Baraza la Mawaziri liliidhinisha rasmi Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, kabla ya kupelekwa bungeni kwa ajili ya kuidhinishwa kisheria.


Prof. Mkumbo alibainisha kuwa dira hiyo itatumika kama mwongozo wa maendeleo wa muda mrefu kwa zaidi ya miaka ishirini ijayo, bila kujali ni serikali gani itakuwa madarakani, kwani dira hiyo ni ya taifa lote.


“Tulichofanya kama taifa ni kuweka bayana tunapotaka kufika. Sasa mjadala wa kisiasa unatakiwa kuangazia namna ya kufanikisha malengo hayo,” alihitimisha.



#dira2050 #maendeleoyataifa #raisamiasuluhu #uzinduzi #tanzaniampya #mustakabalwataifa #kitilamkumbo #dodoma2025

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.